'
Tuesday, January 28, 2014
MCD HATUNAYE
MPIGA tumba namba moja katika muziki wa dansi hapa nchini, Soud Mohamed 'MCD' wa Twanga Pepeta, amefariki dunia usiku huu mjini Moshi.
MCD alikuwa huko kwa zaidi ya miezi miwili akiugua na hali yake ilikuwa inaendelea vizuri lakini hali ikabadilika usiku huu na kuaga dunia.
Msemaji wa Twanga Pepeta, Hassan Rehani ameithibitishia Saluti5 kuwa MCD amefariki dunia.
Wiki iliyopita MCD aliongeana Saluti5 na kusema anaendelea vizuri na kwamba ile hatua ngumu ya dozi kali ya kifua kikuu alikuwa ameshaivuka na sasa amebadilishiwa dawa.
MCD aliongea kwa matumaini makubwa kuwa atarejea jukwaani muda si mrefu.
Majuzi MCD aliomba nauli ya kurejea Dar kwa uongozi wa Aset, jambo ambalo lilitekelezwa haraka na pengine kama siku zake za kuishi duniani zilikuwa bado zipo japo kwa wiki moja mbele, MCD angeaga dunia akiwa Dar es Salaam.
Katika uhai wake bendi zingine alizozitumikia MCD ni na Diamond Sound, Mashujaa Band.
Kwa mujibu wa mkurugenzi wa Aset, Asha Baraka, mpiga tumba wa Twanga Pepeta, Soud Mohamed “MCD” aliyefariki Jumatatu (jana) usiku, mauti yalimfika mara tu baada ya kufika kwenye mlangowa hospitali ya KCMC Moshi.
Akiongea na Saluti5 muda mfupi baada ya taarifa za msiba, Asha Baraka alisema hadi mchana wa leo (Jumatatu) MCD alikuwa kwenye hali nzuri, lakini baadaye hali ikaanza kubadilika.
Asha Baraka anasema dada wa marehemu amemjulisha kuwa ilipofika usiku MCD aliendelea kujiskia ovyo na wakaamua kumkimbiza hospitali ya KCMC.
Lakini kwa mujibu wa maelezo ya dada huyo kupitia kwa Asha Baraka, MCD alifariki mara tu walipofika kwenye mlango wa hospitali hiyo.
Mwili wa MCD umehifadhiwa katika vyumba vya kuhifadhia maiti hospitalini hapo.
MCD alikuwa Moshi ambako ndiko nyumbani kwao alikozaliwa kwa ajili ya kujiuguza maradhi ya kifua kikuu.
IMETOLEWA KUTOKA BLOGU YA SALUTE 5.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment