'
Monday, January 6, 2014
SIMBA HIYOOO ROBO FAINALI KOMBE LA MAPINDUZI
SIMBA SC imefanikiwa kufuzu kucheza robo fainali ya michuano ya Kombe la Mapinduzi, kufuatia ushindi wa bao 1-0 dhidi ya KMKM ilioupata juzi
usiku kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Kwa matokeo hayo, Simba SC inamaliza katika nafasi ya pili kwenye Kundi B, ikiwa na pointi saba, mabao mawili ya kufunga na haijafungwa, nyuma ya KCC ya Uganda yenye pointi saba pia, mabao sita ya kufunga na mawili ya kufungwa.
Hadi mapumziko, tayari Simba SC walikuwa mbele kwa bao hilo moja lilifungwa na Amri Ramadhani Kiemba kwa kichwa, akiunganisha krosi maridadi ya Ali Badru Ali dakika ya tano.
Kocha Mcroatia Zdravko Logarusic akiiongoza timu kwa mara ya kwanza kwenye mashindano haya tangu arejee kutoka mapumzikoni, alifanya mabadiliko makubwa katika kikosi cha kwanza leo, akiwapanga wachezaji wengi wa benchi.
Hata hivyo, wachezaji hao hawakumuangusha kwa kucheza vizuri na kama wangekuwa makini zaidi wangeweza kuondoka na mabao zaidi kipindi cha kwanza.
Kipindi cha pili, KMKM inayofundishwa na Ali Bushiri ilicharuka na kukaribia kufunga mara kadhaa, lakini hata hivyo bahati haikuwa yao na hadi kipyenga cha kuhitimisha mchezo kinapulizwa, walilala 1-0.
KMKM sasa inasubiri mustakabali wake wa kusonga mbele katika nafasi mbili maalum kwa makundi yote, kuungana na timu sita zitakazofozu moja kwa moja kutoka makundi hayo.
Simba SC; Yaw Berko, William Lucian ‘Gallas’, Omar Salum/Miraj Athumani, Gilbert Kaze, Donald Mosoti/Joseph Owino, Abdulhalim Humud, Uhuru Suleiman/Said Ndemla, Amri Kiemba, Betram Mombeki/Zahor Pazi, Ali Badru na Edward Chistopher/Adeyoum Saleh.
KMKM; Mudathir Khamis, Pandu Hajji, Haidhurun Juma, Khamis Ali, Iddi Kambi, Ibrahim Hatibu, Nassor Omar/Hajji Simba, Maulid Kapenta, Vincent Kamanya na Machano Abdallah.
Hatua ya michuano hiyo ilihitimishwa jana kwa mchezo wa mwisho wa Kundi C, ambapo Azam FC iliilaza Ashanti United bao 1-0 Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Bao pekee la Azam leo limefungwa na Mganda, Brian Umony dakika ya 60, akiunganisha krosi ya Kipre Tchetche kutoka wingi ya kulia.
Kwa matokeo hayo, Ashanti inayofundishwa na kocha mkongwe, Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibaden’ inaaga mashindano haya. Ashanti ilihitaji sare tu katika mchezo wa leo ili ifuzu Robo Fainali, lakini imalambwa kidude.
Timu zilizofanikiwa kuingia Robo Fainali ni Azam FC na Tusker ya Kenya kutoka Kundi C, Simba SC na KCC ya Uganda kutoka Kundi B, URA ya Uganda, Chuoni, Cloves Stars na KMKM.
Robo Fainali zitachezwa Jumatano, Tusker na URA Saa 8:00 mchana na Azam FC na Cloves Saa 10:00 jioni Uwanja wa Gombani Pemba na Uwanja wa Amaan, mechi ya kwanza itakuwa kati ya KCC na KMKM Saa 10:00 na Simba SC na Chuoni Saa 2:00 Usiku.
Wakati huo huo, Mbeya City imefungishwa virago Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar, baada ya kufungwa bao 1-0 na URA ya Uganda Uwanja wa Gombani, Pemba jioni ya leo.
Kwa matokeo hayo, Mbeya City inaaga mashindano hayo kwa pointi yake moja iliyovuna kutokana na sare na Clove Stars, huku URA ikiungana na Chuoni iliyotoka sare ya 2-2 na Clove kusonga mbele Robo Fainali moja kwa moja kutoka Kundi A.
Katika mechi ya awali ya Kundi C, Uwanja wa Amaan, Tusker ya Kenya ilikata tiketi ya Robo Fainali pia baada ya kuifunga Spice Stars mabao 2-0, hivyo inaungana na Azam FC kufuzu moja kwa moja Robo Fainali kutoka kundi hilo.
Clove yenye pointi mbili, inaungana na KMKM na Ashanti United zenye pointi moja moja kuwania nafasi mbili za timu zilizomaliza na wastani mzuri katika nafasi ya tatu kutoka makundi yote, ili kuingia Robo Fainali.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment