Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa
Chama cha Mapinduzi (CCM), Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amepokea kwa
mshtuko mkubwa na huzuni nyingi taarifa za kifo cha ghafla cha Mheshimiwa
Kepteni John Damian Komba, Mbunge wa Jimbo la Nyasa, Mjumbe wa Halmashauri Kuu
ya taifa ya CCM na msanii hodari sana wa kizazi chake.
Katika salamu zake za
rambirambi kwa Spika wa Bunge, Mheshimiwa Anne Semamba Makinda na Katibu Mkuu
wa CCM, MheshimiwaAbdulrahman Kinana, Mheshimiwa Kikwete amesema: “Nimepokea
kwa mshtuko mkubwa na huzuni nyingi taarifa za kifo cha ghafla cha Mheshimiwa Kepteni
John Komba, ambacho nimejulishwa kuwa kimetokea mchana wa leo, Jumamosi,
Februari 28, 2015, kwenye Hospitali ya TMJ, Dar es Salaam.”
“Kwa hakika, sina
maneno ya kutosha kuelezea kwa fasaha hasara ambayo taifa letu na chama chetu
kimepata kutokana na kifo cha Kepteni Komba. Taifa letu limepoteza hazina kubwa
na mtu muhimu. Nimemjua Kepteni Komba kwa muda mrefu sana, nimefanya naye kazi. Alikuwa
msanii ambaye kiwango chake cha usanii kilikuwa hakipimiki, alikuwa na sifa
kubwa za uongozi, alikuwa mpenzi, mzalendo na mtu mwaminifu sana kwa taifa lake
na katika jambo lolote aliloliamini.,” amesema Rais Kikwete katika salamu hizo
na kuongeza:
“Akiwa mwalimu,
lakini hasa akiwa Mlinzi wa Taifa katika Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ),
Kepteni Komba alithibitisha sifa zake kama mlinzi wa taifa kwa kipaji chake cha
kutunga na kuimba nyingi za kuhamamisha wanajeshi wetu katika ulinzi wa nchi yao.
Alikuwa na uwezo mkubwa wa kisanii kutunga nyimbo za aina zote – ziwe za
maombolezo, ziwe za kutoa hamasa, ziwe za makaribisho, ziwe za kampeni za
kisiasa na kijamii ama ziwe za kampeni maalum.”
“ Mheshimiwa Komba
alikuwa Mbunge hodari sana na wananchi wa Nyasa wamepoteza mtetezi wa uhakika.
Mheshimiwa Komba alikuwa mcheshi, aliyependa sana utani na alikuwa na uongozi
mkubwa wa kutambua na kulea vipaji vya sanaa na wasanii kama alivyothibitisha
katika kuanzisha na kulea Kikundi cha Tanzania One Theatre (TOT) na kabla ya
hapo .”
“Kupitia kwenu
Waheshimiwa, naomba mnifikishie salamu zangu za dhati kabisa kwa Wabunge wote
ambao wameondokewa na mwenzao na wananchi wa Jimbo la Nyasa na Mkoa wote wa
Ruvuma ambao wamepoteza mwakilishi na kiongozi wao. Ndani ya Chama chetu,
naomba salamu zangu ziwafikie wanachama wetu wote kwa kupoteza mwanachama
mwenzao, ziwafikie viongozi na hasa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ambayo
imepoteza mwakilishi mwenzao na wasanii wote wa Tanzania One Theatre (TOT) ambao
Kiongozi wao ameondoka duniani,” amesema Rais na kumalizia:
Naungana na
wanafamilia kuomboleza kifo cha rafiki yetu, ndugu yetu na kiongozi mwenzetu.
Napenda wanafamilia wajue kuwa natambua uchungu wao katika kipindi hiki na
tahayari yao ya kuondokewa na mhimili wa
familia. Niko nao katika maombolezo na katika kumwomba Mwenyeji Mungu aiweke
peponi roho ya Marehemu Kepteni John Damian Komba. Amen.”
No comments:
Post a Comment