KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, March 15, 2015

MKUTANO MKUU TFF WAMALIZIKA SALAMA NA KWA AMANI


Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) jana limefanya Mkutano Mkuu wa Mwaka katika ukumbi wa Morogoro hoteli ya mjini Morogoro ambapo mgeni Rasmi alikua ni mkuu wa mkoa wa Morogoro Dr Rajabu Rutengwe.

Katika hotuba yake kwa wajumbe wa mkutano huo, Dr Rutengwe aliushukuru uongozi wa TFF nchini kwa kuweza kuandaa mkutano mkuu mzuri na wa kisasa ambao pia ulifanyikia katika mkoa wake wa Morogoro.

Akiongea na wajumbe wa mkutano mkuu Dr Rutengwe alisema, TFF ina changamoto ambazo inapaswa kuzifanyia kazi kwa kushirikiana na wadau wa mpira wa miguu nchini kwa ujumla, changamoto hizo ni kukosekana kwa wataalamu wa vyakula, wataalamu wa tiba na wataalamu wa saikolojia.

Dr Rutengwe aliomba TFF kwa kushirikiana na serikali inapaswa kuandaa wataalamu wengi wa masuala hayo ili kuweza kuendana na mahitaji ya kuwaanda wanamichezo bora ambao watakua tayari kwa ushindani na sio ushiriki.

Aidha mkuu wa mkoa huyo aliipongeza Kamati ya Utendaji ya TFF kwa kuupa mkoa wa Morogoro uenyeji wa mkutano mkuu ambapo pia umefanyika na  malengo kufanikiwa kwa asilimia mia moja, na kusema kwa niaba ya serikali ya mkoa wapo tayari kupokea tena mwaliko wa uenyeji wa mikutano mbalimbali ya TFF.

Mkutano ulijadili Ajenda za kawaida ambazo ni Kufungua Mkutano ni Uhakiki wa Wajumbe,  Kuthibitisha Muhtsari wa Mkutano Mkuu uliopita, Yatokanayo na Mkutano uliopita, Hotuba ya Rais, ripoti kutoka kwa Wanachama,  Kuthibitisha ripoti ya utekelezaji wa Kamati ya Utendaji.

Zingine ni Kuthibitisha ripoti ya Ukaguzi wa Hesabu 2013, Kuthibitisha ripoti ya Kamati ya Ukaguzi wa Hesabu, Kupitisha bajeti ya 2015, Marekebisho ya Katiba,  Mengineyo na  Kufunga Mkutano.
Kwa mara ya kwanza Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TFF limepata bendera yake ambayo ilipitishwa na mkutano mkuu na asubuhi ya jumapili Machi 15 mwaka huu, imepandishwa kwa mara ya kwanza Morogoro hoteli.
Aidha wajumbe wa mkutano mkuu pia wamepitisha azimio la kuanzishwa kwa mfuko wa maendeleo ya mpira wa miguu nchini (FDF), ambapo kutaundwa kamisheni maalum itakayoshugulikia suala hilo.
Lengo la kamisheni hiyo ni kuisaidia TFF kuandaa na kuratibu mipango ya maendeleo ya soka la watoto, vijana, wanawake nchini na kuviwezesha vyama vya soka vya mikoa (FA), vyama shiriki vya TFF kujiendesha katika shughuli mbalimbali za maendeleo ya soka la vijana.
Pia mkutano mkuu huo ulitoa azimio la kuitaka serikali itoe msamaha wa kodi kwa vifaa vya michezo hasa vinavyotumika kufundishia watoto michezo.
Mkutano huo ulihudhuriwa na wajumbe 125 na kati yao wajumbe watano ni wanawake.
Kikao kijacho cha mkutano mkuu kitafanyika kati ya mwezi Novemba na Disemba mwaka huu.


No comments:

Post a Comment