'
Thursday, March 19, 2015
YANGA KWA RAHA ZAO, SIMBA YALE YALE
YANGA jana iliwapa raha mashabiki wake baada ya kuichapa Kagera Sugar mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ushindi wa Yanga katika mechi hiyo ya ligi kuu ya Tanzania Bara, umeiwezesha kufikisha pointi 34 na pia kulipa kisasi cha kufungwa bao 1-0 na Kagera Sugar, katika mechi ya awali iliyochezwa mjini Bukoba.
Iliwachukua Yanga dakika saba kupata bao la kwanza lililofungwa kwa njia ya penalti na Simon Msuva baada ya kuchezewa rafu mbaya ndani ya eneo la hatari. Kipa Andrew Ntila alishindwa kuzuia penalti hiyo.
Amisi Tambwe aliiongezea Yanga bao la pili dakika ya 15 baada ya kupokea pasi kutoka kwa Mrisho Ngasa, aliyekuwa akihaha uwanja mzima kusaka mabao.
Beki wa zamani wa Simba, Salum Kanoni, aliifungia Kagera Sugar bao la kujifariji kwa njia ya penalti dakika ya 40 baada ya Hussein Javu kumchezea rafu Atupele Green ndani ya eneo la hatari.
Wakati huo huo, timu kongwe ya Simba jana iliwakera na kuwapa unyonge mashabiki wake baada ya kupokea kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Mgambo Shooting kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Kutokana na kipigo hicho, Simba imebaki kwenye nafasi ya tatu ikiwa na pointi 29, nyumba ya Yanga na Azam.
Katika mechi hiyo iliyohudhuriwa na mashabiki lukuki, Simba ilizidiwa kila idara na wapinzani wao, hasa kipindi cha pili.
Shambulizi la kushtukiza lililofanywa na Mgambo kwenye lango la Simba dakika ya 44, liliiwezesha kupata bao la kwanza lililofungwa na Ali Nassoro kwa shuti kali lililomshinda kipa Ivo Mapunda.
Simba ilipata pigo dakika ya 63 baada ya kipa wake, Ivo Mapunda kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kosa la kumchezea rafu mbaya Salim Azizi ndani ya eneo la hatari.
Kufuatia Mapunda kutolewa, Simba ililazimika kumtoa Ramadhani Singano na kumuingiza kipa namba mbili, Manyima Peter.
Mgambo ilipata bao la pili dakika ya 66 lililofungwa na Mwalimu Busungu kwa njia ya penalti.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment