'
Sunday, March 1, 2015
MWILI WA KEPTENI KOMBA KUSAFIRISHWA KESHO KWENDA SONGEA, ALITABIRI KIFO CHAKE, ALIAGIZA MWILI WAKE UPITISHWE MBAMBABAY
NA DUSTAN NDUNGURU SONGEA
MWILI wa mbunge wa jimbo la Mbinga magharibi kapteni John Komba aliyefariki jana katika hospitali ya TMJ jijini Dar es salaam unatarajiwa kuwasili kesho mjini Songea,mkoani Ruvuma tayari kwa mazishi.
Akiongea na uhuru mwenyekiti wa CCM wa mkoa huo Oddo Mwisho alisema kuwa mwili wa marehemu unatarajiwa kuwasili uwanja wa ndege wa mjini hapa kesho majira ya mchana ambapo baadaye utapelekwa moja kwa moja ofisi za CCM mkoa kwa ajiri ya wananchi kutoa heshima zao za mwisho.
Alisema baada ya wananchi wa manispaa ya Songea kupata fursa ya kuaga mwili utasafirishwa hadi katika kijiji cha Lituhi kilichopo wilayani Nyasa ambako alizaliwa na kwamba mazishi yanatarajiwa kufanyika februari 3 mwaka huu.
Mwisho alisema viongozi mbalimbali wa kitaifa wanatarajiwa kuanza kuwasili mkoani humo kwa ajiri ya kushiriki mazishi kuanzia leo na kwamba maandalizi yanaendelea kufanyika kwa ajili ya kufanikisha shughuli hiyo.
Alisema wilaya ya Nyasa imepata pigo kubwa baada ya kuondokewa na viongozi wake wawili katika kipindi cha siku mbili ambapo kabla ya kifo cha Komba asubuhi ya februari 27 mwaka huu aliyekuwa katibu wa CCM wa wilaya ya Nyasa Rhoda George alifariki dunia katika hospitali ya mkoa wa Iringa ambako alilazwa kutokana na kusumbuliwa na maradhi na kwamba februari 28 kapteni Komba ambaye pia ni mjumbe wa NEC kupitia wilaya hiyo alifariki dunia.
Alisema baada ya kupokea taarifa za kufariki kwa katibu huyo wa chama,Kapt.Komba alituma shilingi laki tano za rambirambi fedha ambazo alizituma kwa mwenyekiti huyo wa mkoa.
"Niliwasiliana naye jana asubuhi kabla sijaondoka Songea kwenda Iringa kwa ajili ya kushiriki mazishi ya katibu wetu wa wilaya ya Nyasa na akaniambia nakutumia shilingi laki tano kama rambirambi"alisema.
Mwisho alisema baada ya kuanza safari ya kuelekea Iringa wote njiani walikuwa wakiwasiliana kwa nyakati tofauti ambapo mara baada ya kufika mjini Iringa alipiga simu ikapokelewa na mtoto wake huku akimweleza baba yake amefariki.
Wakati huohuo mwenyekiti wa wazazi wa wilaya ya Nyasa Frank Ligola alisema Kapt.Komba wakati wa kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa zilizofanyika desemba mwaka jana katika kila mkutano alisikika akisema maneno ambayo ni kama yalikuwa yakitabiri kifo chake ambapo alidai akifa maiti yake ipitishwe kwanza Mbamba bay kabla ya kwenda kuzikwa kijijini kwake Lituhi.
"Unajua wakati mwingine ni kama alikuwa akitabiri kifo chake wakati wa kampeni za uchaguzi alisema nikifa maiti yangu itapitishwa hapa Mbamba bay kwanza na kuzikwa itakuwa Lituhi"alisema Ligola.
Hata hivi novemba mwaka 2005 mara baada ya kuchaguliwa kuwa mbunge wa jimbo la Mbinga magharibi Kapt.Komba akiwa kijijini kwake Lituhi aliwaambia waandishi wa habari kuwa atakuwa mbunge wa jimbo hilo kwa kipindi cha miaka kumi,ambapo tangu wakati huo mpaka mwaka huu alikuwa akitimiza mwaka ambao alijitabiria atahitimisha safari zake kama mbunge.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment