'
Tuesday, March 17, 2015
AZAM YAITUNGUA NDANDA UNITED 1-0, YAREJEA KILELENI LIGI KUU
Timu ya Azam FC imerejea killeni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kufuatia ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ndanda FC ya Mtwara Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam jioni ya leo.
Ushindi huo ambao ni sawa na kisasi baada ya Azam FC kufungwa pia 1-0 na Ndanda katika mchezo wa mzunguko wa kwanza, unaifanya timu hiyo ya Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa na familia yake ifikishe pointi 33 baada ya kucheza mechi 17.
Mabingwa hao watetezi, sasa wanaizidi Yanga SC kwa pointi mbili, ambayo hata hivyo mchezo mmoja mkononi, Jumatano ikitarajiwa kumenyana na Kagera Sugar Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ikiongozwa na kocha Mganda, George ‘Best’ Nsimbe kwa mara ya pili mfululizo baada ya kufukuzwa kwa Mcameroon, Joseph Marius Omog, Azam FC ilipigana kiume kupata ushindi huo.
Sifa zimuendee Didier Kavumbangu aliyefunga bao lake la 10 dakika ya 24 katika Ligi Kuu msimu huu na la 16 jumla tangu ajiunge na Azam FC akiwa anaichezea katika mechi ya 30 leo.
Kavumbangu, mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi, alifunga bao hilo kwa guu lake la kulia akimalizia pasi ya mfungaji bora wa misimu miwili iliyopita Ligi Kuu, KIpre Herman Tchetche.
Pamoja na ushindi huo, Azam FC ilipata upinzani mkali kutoka kwa Ndanda FC ambao wamepanda Ligi Kuu msimu.
Kikosi cha Azam FC kilikuwa; Aishi Manula, Shomary Kapombe, Erasto Nyoni, Aggrey Morris, Serge Wawa, Mudathir Yahya, Himid Mao, Frank Domayo/John Bocco dk57, Didier Kavumbangu, Kipre Tchetche/Amri Kiemba dk82 na Brian Majwega.
Ndanda FC; Wilbert Mweta, Aziz Sibo, Paul Ngalema, Hemed Kihoja, Cassian Ponela, Zablon Raymond, Jacob Massawe, Ibrahim Mwaipopo/Iddi Kulachi dk57, Nassor Kapama/Gideon Benson dk72, Masoud Ally na Stahmili Mbonde/Kiggi Makassy dk84.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment