KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, March 9, 2015

OKWI APELEKA KILIO JANGWANI


BAO lililofungwa na mshambuliaji Emmanuel Okwi dakika ya 51, jana liliiwezesha Simba kuwatambia watani wao wa jadi Yanga, kwa kuwachapa bao 1-0 katika mchezo wa marudiano wa ligi kuu ya Tanzania Bara.

Katika mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Okwi alifunga bao hilo kwa shuti la umbali wa mita zipatazo 25 baada ya kuwazidi mbio mabeki wawili wa Yanga na kumpima kipa Ally Mustafa Barthez, aliyekuwa ametoka langoni.

Ushindi huo umeiwezesha Simba kuendeleza ubabe kwa Yanga katika mechi walizokutana hivi karibuni. Walipokutana mwaka jana katika mechi ya Nani Mtani Jembe, Simba iliichapa Yanga mabao 2-0.

Katika mechi hiyo, vijana wa Simba walionyesha soka ya kiwango cha juu hasa dakika za mwisho kutokana na kugongeana pasi nyingi bila wachezaji wa Yanga kugusa mpira.

Washambuliaji Simon Msuva, Mrisho Ngasa, Amisi Tambwe na Danny Mrwanda walikuwa mwiba katika ngome ya Simba, lakini umaliziaji wao mbovu uliwakosesha mabao.

Yanga ilipata pigo kipindi cha pili baada ya kiungo wake Haruna Niyonzima kutolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya kuonyeshwa kadi ya pili ya njano baada ya kubutua mpira huku mwamuzi akiwa amepuliza filimbi ya kuotea.

No comments:

Post a Comment