KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, March 18, 2015

FRANCIS CHEKA ABADILISHIWA ADHABU, APEWA KIFUNGO CHA NJE


MAHAKAMA ya  Hakimu Mkazi mkoa wa Morogoro, jana  ilimbadilishia adhabu ya kifungo cha miaka mitatu jela , bondia  wa ngumi za kulipwa nchini, Francis Cheka, ambapo sasa atatumikia kifungo cha nje.

Sambamba na hilo, Cheka atatakiwa kulipa faini ya sh milioni moja kama ilivyoamuliwa awali na mahakama hiyo.

Aidha, Cheka atatakiwa  kutumikia kifungo cha saa  nne  kwa siku, kwa  kufanya shughuli katika taasisi za umma, ikiwemo kwenye ofisi ya mkuu wa mkoa, mkuu wa wilaya na maeneo ambayo atakuwa akipangiwa.

Kulingana  na sheria namba 6 ya mwaka 2002 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2004 inayomtaka  mfungwa kufanya kazi saa nne bila malipo katika taasisi za umma, imemwezesha bingwa wa dunia wa uzito wa kati
(WBF) Cheka, kutumikia kifungo cha nje badala ya gerezani kama ilivyokuwa hukumu yake ya awali.

Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Morogoro, Saidi Msuya,alidai mahakamani hapo kuwa  kutokana na kutiwa hatiani kwa kosa la kumpiga na kumsababishia maumivu meneja wa baa yake, Bahati Kibanda, sheria hiyo ndio  imemwezesha bondia huyo kutumikia kifungo chake  nje ambapo atatakiwa kufanya kazi kwenye taasisi za umma.

Februari 2, mwaka huu, Cheka alihukumiwa kwenda jela miaka mitatu na kulipa faini ya sh.  milioni moja, ambapo alidaiwa  kutenda kosa hilo kwa kumpiga Bahati, aliyekuwa meneja wa baa inayojulikana kwa jina la Vijana Social Hall.

Kutokana na uadilifu wa Cheka akiwa jela,ustawi wa jamii ulitoa pendekezo la kupunguziwa adhabu baada ya kuridhika na mwenendo wa tabia yake akiwa gerezani.

Kwa mujibu wa sheria ya Magereza namba 34 ya mwaka 1967 kifungu cha 51 kilichofanyiwa marekebisho ya sheria namba  9 mwaka 2002 kinampa uwezo wa mkuu wa gereza kuomba kupunzwa kwa adhabu kwa mfungwa.

Kifungu hicho  cha sheria kinamruhushu mkuu wa gereza kuiomba ofisi ya ustawi wa jamii kubadilisha au kukungaza adhabu kwa mfungwa endapo tu itaridhika na tabia ya mfungwa gerezani.

Baada ya ustawi wa jamii kupokea ombi hilo na kuitarifu mahakama, ambayo ilitoa hukumu kwa mfungwa na mfungwa kuanza kutumikia kifungo cha nje kwa kufanya shughuli za kijamii.

Afisa Huduma ya Jamii, Yusufu Ponera, alisema Cheka ni miongoni wa watu 50 walioombewa na mkuu wa gereza kupunguziwa adhabu baada ya kuonyesha tabia nzuri gerezani.

Kifungo cha Francis Cheka kinatarajiwa kumalizika  Februari 1 2017. Katika kipindi hiki, Cheka hatakiwi kufanya uharifu wowote wala kutoka nje ya mkoa bila taarifa.

Hata hivyo, katika hali isiyo ya kawaida, bondia huyo baada ya kutoka mahakamani hapo, aliomba kutoongea lolote wala kupigwa picha, jambo lililowashangaza baadhi ya watu waliohudhuria mahakamani hapo.

"Wana Morogoro tukiungana na Watanzania wengine nchini, tunatoa shukrani zetu za dhati kwa wale wote walioshirikia kwa namna moja au nyingine kuhakikisha Cheka ameachiwa huru, Mungu mkubwa,’’ alisema Rashid  Matesa.

Hata hivyo, wadau hao wa michezo mkoa wa  Morogoro walimtaka Cheka kuhakikisha anatumikia kifungo hicho cha nje kwa uadilifu hadi afikie tamati ili kutoa imani kwa vyombo vya dola.

No comments:

Post a Comment