KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, September 22, 2011

YANGA RAHA TUPU

HARUNA Niyonzima





MABINGWA wa soka wa Tanzania Bara, Yanga jana walituliza mzuka wa mashabiki wa klabu hiyo, baada ya kuifunga Villa Squad mabao 3-2 katika mchezo wa Ligi Kuu uliochezwa kwenye uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.
Mashabiki wa Yanga waliofurika kwenye uwanja huo uliopo nje kidogo ya Dar es Salaam, walitoka uwanjani roho kwatu baada ya kushuhudia timu hiyo ikicheza soka ya kuvutia na kupata ushindi huo ulioifanya kufikisha pointi tisa katika mechi saba ilizocheza.
Yanga ilianza mchezo kwa kasi na mshambuliaji wa kimataifa wa Ghana, Kenneth Asamoah, alikosa bao dakika ya 10 kabla ya Villa Squad kujibu shambulizi hilo dakika ya 11 na kufanikiwa kufunga bao kupitia kwa winga wa zamani wa timu hiyo, Nsa Job aliyepokea pasi ya Mohamed Kijuso.
Kuingia kwa bao hilo kuliamsha hasira za Yanga, ambayo ilijipanga vizuri na kusukuma mashambulizi langoni mwa Villa Squad. Juhudi zao zilizaa matunda dakika ya 15 baada ya kiungo wa kimataifa wa Rwanda, Haruna Niyonzima kufunga kwa mkwaju wa adhabu ndogo.
Dakika ya 27, Yanga ilizidisha kasi ya mchezo na kupata bao la pili kupitia kwa Asamoah, aliyefunga baada ya kupata pasi ya winga, Idrissa Senga. Nurdin Bakari alikosa bao dakika ya 36 licha ya kubaki na kipa Mohamed Bambino kabla ya Asamoah kupiga shuti nje dakika ya 43.
Kipindi cha pili timu hizo zilishambuliana kwa zamu kabla ya Villa Squad kupata pigo dakika ya 57 baada ya mchezaji wake, Stamili Mbonde kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kosa la kumtolea lugha mbaya mwamuzi Ibrahim Kidiwa kutoka Tanga.
Yanga ilipata bao la tatu lililofungwa na Hamis Kiiza, aliyeingia kuchukua nafasi ya Shamte Ally dakika ya 63, akiunganisha mpira wa krosi ya Senga. Villa Squad ilipata bao la pili kupitia kwa Kigi Lusekelo dakika ya 72 kwa shuti kali.
Ushindi huo umeifanya Yanga kupoza machungu baada ya kufanya vibaya katika mechi za awali, ambapo ilianza ligi vibaya kwa kuchapwa bao 1-0 na JKT Ruvu, ilitoka sare 1-1 na Moro United, ilitoka suluhu na Mtibwa Sugar, ilitoka sare 1-1 na Ruvu Shooting, ilishinda 2-1 dhidi ya African Lyon kabla ya kuchapwa 1-0 na Azam.
Yanga: Yaw Berko, Shadrack Nsajigwa, Oscar Joshua, Nadir Haroub, Chacha Marwa, Nurdin Bakari, Shamte Ally/Hamis Kiiza, Haruna Niyonzima, David Mwape, Kenneth Asamoah/ Rashid Gumbo na Idrissa Senga.
Villa Squad: Mohamed Bambino, Haruna Shamte/Evarist Maganga, Yassin Juma, Shai Mpala, Mohamed Lupatu, Zuebr Dabi, Mussa Nampaka, Stamil Mbonde, Mohamed Kijuso, Nsa Job na Lameck Dayton/Kigi Lusekelo. 72
Kutoka Tanga, mwandishi Sophia Wakati, anaripoti kuwa timu ya Azam ilitoka uwanja wa Mkwakwani kifua mbele baada ya kuilaza Coastal Union bao 1-0 lililofungwa na John Bocco dakika ya 32 kwa mpira wa kichwa.

No comments:

Post a Comment