KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, September 9, 2011

Simba yatesa, Yanga nywii


Na Sophia Wakati, Tanga na Mwandishi Wetu, Morogoro
SIMBA jana iliendelea kung’ara katika michuano ya soka ya ligi kuu ya Tanzania Bara baada ya kuichapa Villa Squad bao 1-0 katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.
Wakati Simba ikiwa imetoka uwanjani na ushindi, mabingwa watetezi Yanga waliendelea kuvurunda baada ya kulazimishwa kutoka suluhu na Mtibwa Sugar katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Ushindi ilioupata Simba, ambao ni wa tatu mfululizo, uliiwezesha kuchupa nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo, ikiwa na pointi tisa baada ya kucheza mechi tatu. JKT Ruvu inaongoza kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa kati yake na Simba.
Katika mechi yake ya kwanza, Simba iliilaza JKT Oljoro mabao 2-0 kabla ya kuichapa Coastal Union bao 1-0.
Dalili za ushindi kwa Simba zilionekana mapema baada ya kulishambulia kwa nguvu lango la Villa Squad kwa lengo la kusaka mabao ya mapema, kupitia kwa Haruna Moshi, Gervas Kago na Ulimboka Mwakingwe, ambao walifumua mashuti makali langoni mwa wapinzani wao.
Jitihada zao zilizaa matunda dakika ya saba baada ya kupata bao pekee, lililofungwa na mchezaji wa kimataifa kutoka Jamhuri ya Kati, Kago aliyefunga kwa shuti baada ya kuunganisha mpira wa krosi uliopigwa pembeni na Haruna Moshi 'Boban'.
Kipindi cha pili kilianza kwa Simba kuongeza kasi langoni mwa Villa Squad, lakini wapinzani wao walisimama kidete kuokoa hatari. Mwakingwe nusura afunge bao dakika 62, lakini shuti lake lilipaa juu ya lango akiwa ana kwa ana na kipa Abbas Nassoro.
Villa Squad imepoteza mchezo wa pili tangu kuanza ligi msimu huu.Ilifungwa mabao 3-0 na Toto African katika mchezo wa ufunguzi kabla ya kulazimisha sare bao 1-1 na Kagera Sugar.
Simba: Juma Kaseja, Said Nassor, Amir Maftah, Juma Nyoso, Victor Costa, Jerry Santo, Haruna Moshi, Shija Mkina, Amri Ramadhani, Gervas Kago na Ulimboka Mwakingwe.
Villa Squad: Abbas Nasoro, Haruna Shamte, Yassin Majota, Shai Mpala, Menrad Mbunguza, Zuberi Dabi, Lameck Mbonde, Mussa Nampaka, Mohamed Binslum, Mohamed Kijuso na Nsa Job.
Katika hatua nyingine, timu ya Yanga jana ililazimishwa kutoka suluhu na Mtibwa Sugar katika mchezo wa ligi kuu uliochezwa Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.
Kwa matokeo hayo, Yanga imefikisha pointi mbili baada ya kucheza michezo mitatu. Ilianza vibaya ligi kwa kuchapwa bao 1-0 na JKT Ruvu kabla ya kutoka sare ya bao 1-1 na Moro United.
Yanga itabidi ijilaumu kwa kushindwa kupata bao, kwani ilifanya mashambulizi mengi kwenye lango la Mtibwa kipindi cha pili, lakini washambuliaji wake, Jerry Tegete, Davies Mwape na Kenneth Asamoah hawakuwa makini.

No comments:

Post a Comment