KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, September 22, 2011

UCHE JOMBO: Nitapambana hadi nipate haki ninayostahili


Aenda mahakamani kudai fidia dhidi ya gazeti lililomchafua

Asema si kweli kwamba alitoa mimba yenye umri wa miezi sita

Asema alipungua uzito sababu ya kucheza nafasi ya mgonjwa wa kansa
LAGOS, Nigeria
MCHEZA filamu nyota wa Nollywood, Uche Jombo ameeleza kukerwa kwake na taarifa zilizoripotiwa hivi karibuni na baadhi ya vyombo vya habari nchini Nigeria kuwa, ametoa mimba yenye umri wa miezi sita.
Akizungumza kwa uchungu wiki iliyopita mjini hapa, Uche alisema habari hizo si tu kwamba zimemkera, bali zimemvunjia heshima na kumjengea taswira mbaya mbele ya jamii.
Uche alisema ni wazi mwandishi wa habari aliyeandika habari hizo, alidhamiria kumdhalilisha na kumpa machungu moyoni.
Alisema habari hizo zimesababisha apatwe na uchungu muda wote huku baadhi ya wakati akitokwa na machozi na aliapa lazima awashughulikie waliomchafua.
“Unafahamu jinsi nilivyoguswa na habari hizi. Nimewahi kulia kwa sababu ya masuala madogo, lakini kwa hili, nimekerwa na mtu huyu na itaendelea kuwa hivi kwa siku nyingi zijazo. Nitamuomba Mungu anikutanishe na mtu huyu na si kumdhuru,”alisema nyota huyo wa Nollywood.
Uche, ambaye hivi karibuni alifanya uzinduzi wa filamu yake mpya ya ‘Damage’ alisema, yupo tayari kupambana na watu waliomchafua hadi pale atakapohakikisha anapata haki anayostahili.
Alisema ameshafungua kesi mahakamani dhidi ya chombo kilichochapisha habari hizo pamoja na mwandishi aliyeziandika kwa sababu ni za uzushi na hazina ukweli wowote.
Uche alisema habari hizo, ambazo zilichapishwa ukurasa wa mbele wa chombo hizo, bado zinaendelea kumfanya asiwe na raha ndio sababu ameamua kutafuta haki yake mahakamani.
“Kwangu mimi, hii ilikuwa skendo kubwa kutokea. Iliniathiri hasa na siwezi kuacha kupambana hadi nitakapopata haki,”alisisitiza mcheza filamu huyo mwenye sura na umbo lenye mvuto huku akitokwa na machozi.
Alisema habari zilizochapishwa na gazeti hilo ni mbaya kuliko zote katika maisha yake na uigizaji wa filamu na kusisitiza kuwa, zilikuwa za kuchukiza na hazikuwa na ukweli wowote.
Uche alisema wakati wa uzinduzi wa filamu yake ya pili ya Holding Hope mwaka jana, alipoteza uzito mwingi kutokana na nafasi aliyocheza ya mgonjwa wa kansa, lakini inashangaza kuona gazeti hilo likiripoti kwamba alitoa uja uzito wa miezi sita na ndio sababu mwili wake ulipungua.
“Habari hizi zimetapakaa kila sehemu duniani. Ukifungua tu mtandao wa Google na kuandika Uche atoa mimba, utaona zaidi ya kurasa 500. Habari hizo karibu ziyavuruge maisha yangu,”alisema.
“Ukweli ni kwamba ilikuwa karibu ziniue na kuchafua kila nilichokifanya katika maisha yangu ya kiusanii. Unaposema mtu fulani ametoa mimba ya miezi sita, husemi tu ametoa mimba, ni sawa na kusema mtu fulani ni muuaji kwa sababu mimba ya miezi sita tayari kiumbe kinakuwa kimekamilika,”aliongeza.
Mwanadada huyo alisema, haelewi kwa nini inafikiriwa kwamba, mwanamke anaweza kupungua uzito kwa sababu ya kutoa mimba.
Uche alizaliwa katika mji wa Enugu uliopo mashariki mwa Nigeria na kukulia katika mjini wa Aba, ambao upo kwenye jimbo la Abia. Ni mhitimu wa masomo ya hesabu na takwimu katika Chuo Kikuu cha Calabar na pia amehitimu masomo ya sayansi ya kompyuta katika chuo kikuu cha Minna kilichopo jimbo la Niger.
Alijitosa kwenye fani ya uigizaji filamu mwaka 1999 na tangu wakati huo amecheza zaidi ya filamu 60. Pia ni mwandishi mzuri wa miswada ya filamu na ameandika miswada ya filamu nyingi, zikiwemo The Celebrity, Games Men Play, Girls in the Hood, A Time to Love , Be my wife, Perfect Planner, Price of Fame na To Love Forever.
Filamu yake ya kwanza kuitengeneza yeye mwenyewe inajulikana kwa jina la Ibinabo. Filamu zingine alizozitengeneza ni pamoja na Nollywood Hustlers, Holding Hope na Damage.
Uche amewahi kushinda tuzo nyingi kutokana na umahiri wake katika kucheza filamu na pia mchango wake katika maendeleo ya fani hiyo nchini Nigeria.

No comments:

Post a Comment