KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, September 22, 2011

Viongozi Yanga wasikwepe lawama timu kuvurunda


HALI imeendelea kuwa si shwari ndani ya klabu ya Yanga, kufuatia timu hiyo kuchapwa bao 1-0 na Azam katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara, iliyochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kipigo hicho kilikuwa cha pili kwa Yanga katika mechi sita ilizocheza hadi sasa katika ligi hiyo. Kabla ya mechi ya jana dhidi ya Villa Squad, Yanga ilikuwa na pointi sita baada ya kushinda mechi moja na kutoka sare mechi tatu.
Ushindi wa Yanga dhidi ya African Lyon wiki iliyopita, ulionekana kuleta ahueni kubwa kwa mashabiki na wanachama wa klabu hiyo, huku vyombo vya habari vikiipamba kwa vichwa mbalimbali vya habari vyenye mvuto, vikiwemo vile vilivyosema ‘Yanga yaanza ligi’ , ‘Timbe aanza kazi’ na ‘Yanga yaona mwezi’.
Lakini kipigo ilichokipata kutoka kwa Azam kimezusha mambo mengine mapya. Wapo wanaoendelea kuamini kuwa, hizo ni hujuma zinazoendelea kufanywa na baadhi ya wachezaji wa klabu hiyo na wengine wameutupia lawama uongozi kwa kushindwa kujali maslahi ya wachezaji.
Pia wapo wanaowatuhumu baadhi ya viongozi wa zamani wa klabu hiyo kwamba, wamekuwa wakiwatumia wachezaji kuuhujumu uongozi wa sasa chini ya Mwenyekiti Lloyd Nchunga ili kuufanya uonekane haufai. Hizo zote ni tetesi.
Vilevile kuna habari kuwa, wachezaji wa Yanga wanaudai uongozi sh. milioni 30 walizopewa na mfadhili mkuu wa zamani wa klabu hiyo, Yusuf Manji baada ya timu hiyo kutwaa ubingwa wa ligi kuu na ule wa Kombe la Kagame. Pia kuna habari kuwa, wachezaji wa Yanga hawajalipwa mishahara yao kwa miezi kadhaa.
Sina hakika na madai hayo ya wachezaji kwa sababu hakuna kiongozi yeyote wa Yanga aliyewahi kukiri hadharani iwapo ni kweli hawajawalipa wachezaji pesa hizo, ambazo ni haki yao. Swali la msingi la kujiuliza ni je, ni kipi kilichoisibu Yanga na kuifanya ivurunde katika mechi hizo za mwanzo za ligi kuu?
Suala la kufungwa kwa Yanga katika mechi za ligi kuu si la ajabu. Timu hiyo kongwe imewahi kufungwa katika mechi kadhaa miaka ya nyuma kama ilivyo kwa watani wao wa jadi Simba, lakini hazikuwahi kutolewa tuhuma kama zinazotolewa sasa.
Kocha Mkuu wa Yanga, Sam Timbe alikaririwa na baadhi ya vyombo vya habari wiki hii akidai kuwa, kuvurunda kwa timu hiyo kumechangiwa kwa kiasi kikubwa na udhaifu wa safu yake ya ushambuliaji.
Timbe alinukuliwa akisema kuwa, washambuliaji wa timu hiyo, wakiwemo maproo wanne, wamekuwa wakifika mara kwa mara kwenye eneo la hatari la timu pinzani, lakini wanashindwa kufunga mabao. Alidai huo ni upungufu katika kitu kinachoitwa uwezo binafsi wa mchezaji.
Lakini baadhi ya wachezaji wa timu hiyo wamemtupia lawama kocha huyo kwa madai kuwa, amekuwa akipanga kikosi chake kwa upendeleo huku akiwapa kipaumbele zaidi baadhi ya wachezaji, hasa maproo, hata kama uwezo wao umeshuka.
Wachezaji hao walisema pia kuwa, kocha huyo amekuwa akiwanyima nafasi ya kucheza baadhi ya wachezaji, ambao wamekuwa wakionyesha uwezo wa juu mazoezini na kusababisha kuwepo kwa makundi mawili ndani ya timu hiyo. Kwamba wale, ambao hawajawahi kucheza hata mechi moja, wamekuwa wakiwachukia wale wanaochezeshwa mara kwa mara.
Inawezekana ni kweli kwamba wachezaji wa Yanga wanaudai uongozi fedha zao, lakini je, kucheza chini ya kiwango ndio suluhisho la kupatiwa fedha hizo? Je, timu itakaposhindwa kupata tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa ama kuteremka daraja, hasara itakuwa kwa nani?
Na ni kwa nini Kocha Timbe apange timu kwa kubagua wachezaji? Iweje kocha huyo ang’ang’anie kuwachezesha baadhi ya wachezaji hata kama uwezo wao ni mdogo?
Yapo maswali mengi ya kujiuliza, lakini majibu wanayo wenyewe wachezaji wa Yanga, uongozi pamoja na benchi la ufundi. Cha msingi ni pande hizo tatu kukutana na kujadiliana ili kujua tatizo ni nini ili waweze kulipatia ufumbuzi.
Kinachotokea hivi sasa kwa Yanga hakina tofauti na kile kinachotokea kwa klabu ya Arsenal katika michuano ya ligi kuu ya England msimu huu. Timu hiyo imevurunda katika mechi zake kadhaa, lakini lawama kubwa zimeelekezwa kwa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Arsene Wenger.
Pamoja na kuvurunda huko, Wenger ambaye amekuwa kocha wa Arsenal kwa miaka 15 sasa, amekaririwa akisema kuwa, hana wasiwasi wa kutimuliwa na kusisitiza kuwa, anaamini ataendelea kubaki klabu hiyo.
Lakini hali ni tofauti kwa Yanga. Kuna tetesi kuwa, kamati ya utendaji ya klabu hiyo huenda ikafikia uamuzi wa kumtimua kutokana na uwezo mdogo aliouonyesha katika kukisuka kikosi cha timu hiyo.
Iwapo ni kweli uongozi wa Yanga umefikia uamuzi huo, inaonekana umesahau kwamba, Timbe ndiye aliyeiwezesha timu kutwaa ubingwa wa ligi kuu dakika za mwisho msimu uliopita na pia kutwaa Kombe la Kagame.
Sasa iweje kocha aliyeiwezesha Yanga kutwaa mataji hayo, aonekane hafai msimu huu kutokana na timu kufanya vibaya katika mechi chache za mwanzo wa ligi? Ni wazi kwamba, lipo tatizo lingine kubwa na Timbe anabebeshwa msalaba usiomuhusu.
Ni vyema viongozi wa Yanga watafakari kwa makini nini kiini cha timu yao kuvurunda katika ligi na kuchukua hatua zinazostahili badala ya kuwabebesha lawama Timbe na wachezaji.
Kama ni kweli wachezaji wanaudai uongozi malipo yao, ni dhahiri kwamba, hilo linaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa kushusha ari yao uwanjani. Mchezaji atachezaje kwa moyo wakati hajalipwa madai yake? Na kwa nini uongozi umeshindwa kuwalipa madai yao, ambayo ni haki yao ya msingi? Tatizo lipo wapi?
Kama ni pesa, tayari Manji alishazikabidhi kwa uongozi. Na kama ni mishahara, inatoka moja kwa moja kwa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), ambayo pia inaidhamini Simba. Sasa tatizo ni nini?
Nawashauri viongozi wa Yanga wasikwepe lawama moja kwa moja. Lazima wawaeleze ukweli watanzania kuhusu sababu za timu yao kuvurunda badala ya kuwabebesha lawama kocha na wachezaji.

No comments:

Post a Comment