MWAKILISHI wa Tanzania katika shindano la Miss Universe 2011, Nelly Kamwelu mwishoni mwa wiki hii anatarajiwa kupanda ulingoni mjini Brasilia nchini Brazil kuwania taji hilo.
Nelly, ambaye ni mshindi wa taji hilo mwaka huu hapa nchini, atapanda jukwaani pamoja na washiriki wengine zaidi ya 100 kutoka nchi mbalimbali duniani.
Habari kutoka nchini Brazil zimeeleza kuwa, Nelly ni miongoni mwa warembo waliofanya vizuri katika hatua za awali za shindano hilo. Hatua hizo ni shindano la mrembo mwenye kipaji na mwanamichezo bora.
Picha kadhaa za mtandao wa Miss Universe zimekuwa zikimuonyesha Mtanzania huyo akishirki katika kucheza soka ya wanawake wakati wa shindano la mwanamichezo bora.
Kadhalika mrembo huyo alitia fora katika shindano la kumsaka mrembo mwenye kipaji kutokana na kuonyesha umahiri mkubwa wa kucheza ngoma za utamaduni za makabila ya Tanzania.
Shindano la Miss Universe ndilo kongwe kuliko yote duniani, likifuatiwa na lile la kumsaka mrembo wa dunia. Mashindano hayo mawili hufanyika kila mwaka.
Nelly ni mrembo wa tano kuiwakilisha Tanzania katika shindano hilo. Wa kwanza alikuwa Flaviana Matata mwaka 2007, ambaye alifanikiwa kuingia hatua ya 15 bora katika shindano la Miss Universe na kushika nafasi ya sita.
Flaviana, ambaye alishiriki kwenye shindano hilo nchini Mexico,aliibuka kuwa kivutio kikubwa kwa mashabiki kutokana na kunyoa nywele zake zote na kubaki upara. Kwa sasa, Flaviana ni mwanamitindo maarufu nchini Marekani.
Amanda Ole Sululu, msichana wa kabila la kimasai kutoka Arusha, aliibuka mshindi wa taji hilo mwaka 2008, lakini hakuweza kufanya vizuri katika shindano la Miss Universe baada ya kutolewa hatua za awali.
Pamoja na kuvurunda katika shindano la dunia, Amanda aliweka rekodi ya kuwa kivutio kwa mashabiki wakati wa shindano la hapa nchini. Kabla ya matokeo kutangazwa wakati wa fainali, mashabiki walilipuka mayowe ya kumshangilia huku wakilitaja jina lake kabla ya jaji mkuu kumtangaza mshindi.
Illuminata James kutoka mkoani Mwanza, aliibuka mshindi wa taji hilo mwaka 2009 na kushiriki kwenye shindano la Miss Universe mjini Nassau, Bahamas.
Hata hivyo, kama ilivyokuwa kwa washiriki wenzake waliotangulia, Illuminata hakuweza kufanya vizuri katika shindano hilo. Alitolewa hatua za awali.
Mwaka jana, taji hilo lilinyakuliwa na Hellen Dausen kutoka mkoani Arusha, ambaye naye alishindwa kufanya vizuri katika shindano la Miss Universe baada ya kutolewa hatua za awali.
Na sasa macho na masikio yote ya watanzania yapo kwa Nelly, ambaye amekabidhiwa dhamana ya kupeperusha bendera ya Tanzania katika mashindano hayo keshokutwa.
Je, Nelly ataweza kufuata nyayo za Flamiana ama atafika mbali zaidi. Tusubiri tuone.
No comments:
Post a Comment