KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, September 22, 2011

Wadau Z'bar walilia udhamini wa TBL

BAADHI ya wadau wa michezo wa Zanzibar wameiomba serikali iruhusu Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) na ile ya Serengeti (SBL) kudhamini michezo visiwani humo.
Wadau hao walitoa ushauri huo mwishoni mwa wiki iliyopita, kufuatia serikali kupokea msaada wa sh. milioni 20 kutoka TBL kwa ajili ya kuwasaidia watu walioathirika kutokana na ajali ya meli ya MV Spice Islander.
Katika ajali hiyo iliyotokea wiki iliyopita eneo la Nungwi, watu zaidi ya 200 walipoteza maisha wakati wengine 600 waliokolewa. Meli hiyo ilikuwa ikitoka Unguja kwenda Pemba.
Wadau hao walisema, iwapo serikali imekubali kupokea msaada wa fedha kutoka TBL, hawaoni kwa nini iizuie kampuni hiyo na zinginezo zinazotengeneza pombe, kudhamini michezo visiwani humo.
“Kwanza tunaipongeza TBL kwa mchango wake huo kwa serikali. Lakini pili tunahoji kwa nini serikali yetu imekubali kupokea msaada huo, lakini inaizuia TBL kudhamini michezo,” alihoji mdau, aliyejitambulisha kwa jina la Issa Jecha.
Mdau huyo alisema, ameshangaa kusikia serikali imekataa kupokea msaada kutoka Vodacom kwa ajili ya kuwachangia wahanga wa ajali hiyo, lakini imepokea msaada huo kutoka TBL.
“Kwa kweli hapo serikali inatuchanganya. Imeikatalia Vodacom kwa sababu iliendesha mashindano ya Miss Tanzania mara tu baada ya ajali. Sasa iweje ipokee msaada wa TBL wakati haitaki matangazo ya pombe?” Alihoji Jecha.
Mdau mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Jacob Masanja alisema, ipo haja kwa serikali kutafakari kwa makini uamuzi wake wa kuzuia udhamini wa kampuni zinazotengeneza pombe katika michezo visiwani Zanzibar.
“Kama kweli serikali imedhamiria kwa dhati kukataa udhamini wa pombe katika michezo, basi isikubali kupokea misaada ya kampuni hizo katika miradi ya maendeleo na ile ya kuchangia matatizo,”alisema.
Alisema huu ni wakati mwafaka kwa serikali kuziruhusu TBL na SBL kudhamini michezo ili kusaidia kuinua viwango mbalimbali vya michezo visiwani humo.
Mdau mwingine aliyejitambulisha kwa jina moja la Samir Habibu alisema, bila udhamini, haitakuwa rahisi kwa Zanzibar kupata maendeleo katika michezo kwa sababu uendeshaji wake ni gharama kubwa.

No comments:

Post a Comment