KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, September 9, 2011

GENEVIEVE: Nimejifunza mengi Miss TZ


MREMBO wa Tanzania wa mwaka jana, Genevieve Emmanuel amesema, amejifunza mengi kutokana na kushikilia taji hilo kwa mwaka mmoja.
Genevieve, ambaye anajiandaa kumkabidhi taji mrembo wa mwaka huu, atakayepatikana keshokutwa, amesema kwa sasa anajiamini zaidi kuliko ilivyokuwa kabla ya kushinda shindano hilo.
Akizungumza na Burudani mjini Dar es Salaam juzi, Genevieve alisema taji hilo limemwezesha kupata uzoefu mkubwa katika mambo mbalimbali.
“Mimi kama Vodacom Miss Tanzania ninayemaliza muda wangu, nimejifunza namna ya kushirikiana na kujichanganya na watu, na pia nimeongeza uwezo wa kujiamini,”alisema.
Genevieve alisema changamoto pekee kubwa aliyoipata ni kukosa ushirikiano mzuri wa wadhamini, hasa katika azma ya kusaidia jamii.
Kutokana na kujitokeza kwa tatizo hilo, mrembo huyo amezishauri kampuni, taasisi na watu binafsi wenye uwezo kifedha, kuwaunga mkono warembo na kuwatumia katika kazi zao.
Akizungumzia ushiriki wake katika shindano la kumsaka mrembo wa dunia mwaka jana, Genevieve alisema japokuwa hakufanya vizuri, anaamini aliipeperusha vyema bendera ya Tanzania.
“Nina hakika niliiwakilisha vizuri nchi yangu ya Tanzania na kupeperusha vyema bendera yetu. Tulikuwa washiriki 105 na mshindi aliyehitajika ni mmoja. Hivyo kwa jumla nami ni mshindi,”alisema.
Alipoulizwa mtazamo wake kuhusu shindano la mwaka huu, Genevieve alisema washiriki wengi ni wazuri na wanakidhi vigezo vinavyotakiwa, lakini uamuzi wa mwisho utakuwa wa majaji.
Alisema anashukuru kwa kumaliza muda wake salama bila kuandamwa na kashfa zozote kama ilivyokuwa kwa baadhi ya warembo waliopita na anamini mrembo mpya atakayepatikana keshokutwa atatekeleza vyema majukumu yake.

No comments:

Post a Comment