'
Friday, September 9, 2011
Mrembo yupi kutwaa taji la Miss TZ kesho?
WAREMBO 30 kutoka mikoa mbalimbali nchini, keshokutwa wanatarajiwa kupanda ulingoni kuwania taji la Vodacom Miss Tanzania 2011 katika shindano litakalofanyika kwenye ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.
Washiriki hao walipata tiketi ya kuwania taji hilo baada ya kufanya vizuri katika mashindano ya mikoa na kanda. Mashindano hayo yalianza Juni mwaka huu na yanafikia tamati kesho.
Mshindi wa taji hilo mwaka huu atazawadiwa gari aina ya Jeep Patriot lenye thamani ya sh. milioni 72. Gari hilo limetolewa na Kampuni ya CFAO Motors na lilionyeshwa kwa warembo hao Jumatatu iliyopita.
Tofauti na mashindano yaliyopita, shindano la mwaka huu lilikuwa na mabadiliko makubwa, ambapo washiriki badala ya kukaa hotelini, walikwenda ndani ya nyumba moja, iliyofahamika kwa jina la Vodacom House.
Wakiwa ndani ya nyumba hiyo, mbali ya kufanya mazoezi ya miondoko ya kwenye steji, washiriki walipata mafunzo mbalimbali kuhusu maisha na jamii kwa ujumla.
Miongoni mwa mafunzo yaliyotolewa kwa washiriki hao ni pamoja na ujasiliamali, kujitambua wao ni nani na pia tahadhari ya ugonjwa hatari wa ukimwi.
Warembo hao pia walipata fursa ya kutembelea vivutio mbalimbali vya kitalii vilivyopo mjini Arusha, kupiga picha na wenyeji, kutembelea vituo kadhaa vya kulea watoto yatima vya mjini Dar es Salaam na kushiriki kwenye maonyesho ya mavazi.
Kwa mujibu wa utaratibu mpya wa mashindano hayo uliobuniwa na Vodacom, shindano la mwaka huu lilitanguliwa na mashindano madogo manne, ambapo washindi walipata tiketi ya kuingia moja kwa moja hatua ya nusu fainali.
Mashindano hayo madogo, ambayo pia hufanyika wakati wa shindano la kumsaka mrembo wa dunia ni ya mrembo mwenye kipaji, mrembo mwenye mvuto wa picha, mrembo mwanamichezo na mwanamitindo bora.
Mshindi wa taji la mrembo mwanamichezo alikuwa Loveness Flavian wakati taji la mrembo mwenye mvuto wa picha lilinyakuliwa na Tracy Mabula. Mwajabu Juma aliibuka mshindi wa taji la mwanamitindo bora wakati Rose Albert alishinda taji la mrembo mwenye kipaji.
Warembo 15 wanatarajiwa kuingia katika hatua ya nusu fainali kabla ya kupatikana warembo watano watakaoingia fainali. Warembo hao watano ndio watakaoulizwa maswali ili kupimwa ufahamu wao juu ya mambo mbalimbali na hatimaye kutangazwa mshindi.
Warembo watakaowania taji hilo mwaka huu, kanda wanazotoka zikiwa kwenye mabano ni Jenifer Kakolaki (Ilala), Leyla Juma (Nyanda za Juu), Mwajabu Juma (Temeke), Mariaclara Mathayo (Mashariki), Cynthia Kimasha (Temeke), Christina William (Nyanda za Juu Kusini), Hamisa Hassan (Kinondoni), Alexia Williams (Ilala), Stacy Alfred (Kaskazini) na Asha Saleh (Mashariki).
Wengine ni Zubeda Seif (Kaskazini), Rose Hubert (Kaskazini), Maua Kimambo (Kati), Glory Samuel (Ziwa), Neema Mtitu (Chuo Kikuu Huria), Atu Daniel (Nyanda za Juu Kusini), Blessing Ngowi (Elimu ya Juu), Weirungu David (Chuo Kikuu Huria), Chiary Masonobo (Chuo Kikuu DSM), Irene Karugaba (Ziwa).
Washiriki wengine ni Delilah Gharib (Kati), Tracy Sospeter (Ziwa), Husna Twalib (Temeke), Loveness Flavian (Mashariki), Christine Mwegoha (Kati), Husna Maulid (Kinondoni), Zerulia Manoko (Kati), Salha Israel (Ilala), Glory Lory (Vyuo Vikuu) na Stella Mbuga (Kinondoni).
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment