KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, September 9, 2011

Kasaloo Kyanga afariki dunia, kuzikwa kesho makaburi ya Sinza



MWANAMUZIKI mkongwe kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Kasaloo Kyanga amefariki dunia.

Kasaloo amefariki dunia leo asubuhi katika hospitali ya Mwananyamala, Dar es Salaam, ambako alikuwa amelazwa siku mbili zilizopita.

Mwanamuziki huyu ni pacha wa mwanamuziki mwingine, Kyanga Songa, ambaye alifariki miaka kadhaa iliyopita akiwa nchini Kenya.

Marehemu Kasaloo atakumbukwa sana kwa vibao vyake mbalimbali alivyowahi kuvitunga na kuviimba akiwa na bendi za Super Matimila, Maquis Original na Tuncat Almasi Orchestra.
Miongoni mwa vibao vilivyompatia umaarufu ni pamoja na Kalubandika, alichokiimba akiwa Maquiz, ambacho jina lake lilitumika sana katika nchi za ukanda wa Afrika Mashariki kuwakebehi wanaume ambao ni laghai wa mapenzi.
Kibao kingine kilichomfanya mwanamuziki huyo aheshimika katika anga la muziki hapa nchini ni Masafa Marefu, alichokiimba akiwa na bendi ya Tancut.

Kasaloo aliletwa hapa nchini kwa mara ya kwanza miaka ya mwishoni mwa 1980 na mmiliki wa bendi ya Super Matimila. Wakati akija nchini, Kasaloo alifuatana na mwimbaji mwenzake kutoka Congo, Skassy Kasambula.

Kwa sasa, Kasambula yupo nchini akitokea Kenya, ambako amekuwa akiishi na kupiga muziki kwa miaka kadhaa sasa. Kasambula alirejea nchini kuja kumuuguza Kasaloo.

Kwa mujibu wa mwanamuziki mkongwe nchini, John Kitime, msiba wa Kasaloo upo nyumbani kwake Manzese jirani na baa ya Sandton na Tip Top na mazishi yake yamepangwa kufanyika kesho kwenye makaburi ya Sinza, Dar es Salaam.

Wadau wa muziki nchini watamkosa marehemu Kasaloo, lakini sauti yake maridhawa na tungo zake tamu zitaendelea kudumu masikioni mwa mashabiki wa muziki.

Mungu alitoa, Mungu ametwaa, jina lake litukuzwe. Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema, peponi.

No comments:

Post a Comment