Viongozi wa timu za Simba na Yanga, Geofrey Nyange Kaburu, kushoto ambaye ni Makamu wa Rais Simba na Mohamed Bhinda, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa Yanga (kulia) wakishindana kupiga danadana kuashiria uzinduzi rasmi wa kampeni ya Nani Mtani Jembe 2 inayoendeshwa na bia ya Kilimanjaro Premium Lager. Uzinduzi huo ni kwaajili ya wadau wa timu hizo ulifanyika jana viwanja vya Leaders jijini Dar es Salaam jana
Viongozi wa timu za Simba na Yanga, Geofrey Nyange Kaburu, kushoto ambaye ni Makamu wa Rais Simba na Mohamed Bhinda, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa Yanga (kulia) wakivuta kamba kuashiria uzinduzi rasmi wa kampeni ya Nani Mtani Jembe 2 inayoendeshwa na bia ya Kilimanjaro Premium Lager. Uzinduzi huo rasmi kwa wadau wa Simba na Yanga ulifanyika jana viwanja vya Leaders jijini Dar es Salaam.Katikati ni Meneja wa bia hiyo, George Kavishe na Mkurugenzi wa Masoko wa TBL, Bi Kushilla Thomas (aliyevaa suruali nyeupe).
Mashabiki wa Timu za Simba na Yanga wakicheza muziki wakati wa uzinduzi wa kampeni ya Nani Mtani Jembe 2 kwa wadau wa timu hizo mbili katika hafla iliyofanyika viwanja vya Leaders jijini Dar es Salaam jana.
Na Mwandishi Wetu
Shindano la ‘Nani Mtani Jembe2’ linalowakutanisha wakongwe wa Soka hapa nchini Simba na Yanga, limeanza kwa kasi msimu huu, baada ya jana kuwepo kwa shamrashamra za aina yake katika uzinduzi rasmi uliofanyika katika viwanja vya Leaders Jijini Dar es Salaam.
Mashabiki lukuki wa timu hizo na viongozi wao jana walijitokeza kwa wingi katika viwanja hivyo katika hafla iliyopambwa na makundi mbalimbali ya timu hizo yaliyokuwa yakitambiana mwanzo mwisho.
Msimu huu wa ‘Nani Mtani Jembe2’ unaoendeshwa na bia ya Kilimanjaro Premium Lager- wadhamini wakuu wa timu hizo, ulishuhudiwa Simba akianza vema katika mchezo wa soka baada ya Mjumbe wake wa Kamati ya Utendaji Said Tully kuwabuziga Yanga bao 1-0 katika mchezo wa kirafiki wa mashabiki wa Simba na Yanga uliokuwa sehemu ya uzinduzi huo.
Katika mchezo huo wa soka ambao ulionekana kuwa na ushindani mkubwa, Simba waliwafunga Yanga iliyoongozwa na nahodha wao Mjumbe wa Kamati ya Utendaji Mohamed Bhinda huku kwa upande wa danadana Bhinda akimshinda Makamu wa Rais wa Simba Geofrey Nyange ‘Kaburu’,huku kwa upande wa kuvuta kamba mashabiki wa tiu hizo wakitoka sare.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti viongozi wa timu hizo ‘Kaburu’ wa Simba pamoja na Mohammed Bhinda wa Yanga wote walianza kujigamba kuhakikisha wanaibuka na kitita cha mil 100 ambacho kimeandaliwa na Kilimanjaro Premium Lager.
Kaburu alisema, Yanga wameonekana wazi kuanza kushindwa, baada ya kuwatembezea kichapo cha bao 1-0 na pia kutoka sare ya kuvutana kamba hasa wakizingatia msimu uliopita wa Nani Mtani Jembe waliwazidi katika kila idara isipokuwa katika kura zilizopigwa na mashabiki ambapo Yanga walipigiwa zaidi kura na kuibuka na kitita cha shilingi milioni 98 kati ya milioni 100.
“Hapa imeonekana tumetoka sare katika kuvuta kamba, ila Yanga kama mnavyowajua wanapenda ubishi, wamevuta kamba wengi zaidi ya sisi lakini tumewaachia tu na msimu huu tutahakikisha tunachukua pesa zote na kuwaachia kifuta jasho tu,’alisema Kaburu.
Naye Bhinda aliwataka wanachama na mashabiki wa Yanga kuhakikisha wanaitendea haki Nani Mtani Jembe2 hii ili Yanga iwagalagaze Simba, kwa kuwa msimu uliopita waliwawaonea huruma Simba na kuwapa nafasi ya kuwafunga mabao 3-1 baada ya kuona wamezidiwa katika kuvutana.
“Sisi bwana hatuna shida na hawa watani zetu ndio maana tukawaleta wachezaji kutoka katika kitovu cha soka Brazil na bila ya kuwaleta sisi Simba wangetoa wapi nafasi ya kuwaona Wabrazil wakisakata kabumbu Tanzania,”alisema Bhinda.
Alisema kwa kila bia ya Kilimanjaro Premium Lager yenye ujazo wa milita 500 ambayo mteja atanunua ataona namba maalum na ataandika jina la timu yake (SIMBA au YANGA) ikifuatiwa na namba hiyo na atatuma kwenda namba 15415 na kwa kufanya hivyo atakuwa amepunguza kiasi cha shilingi 10,000 kwenye akaunti ya klabu pinzani na kuiongezea klabu yake kiasi hicho cha sh. 10,000.
“Msimu huu ni wa kipekee sana maana tumeona bora atakayefungwa siku ya mechi ya Nani Mtani Jembe walau apate kifuta jasho cha sh mil 5 huku mshindi akipata milioni 15. Klabu itanufaika, wachezaji watanufaika na mashabiki watanufaika. Sasa ni kazi kwenu viongozi kuwahamasisha mashabiki wa timu zenu,”alisema Kavishe.
No comments:
Post a Comment