'
Tuesday, October 28, 2014
POLISI AFRIKA KUSINI WATANGAZA DAU KWA ATAKAYETOA TAARIFA ZA WATU WALIOMUUA SENZO MEYIWA
JOHANNESBURG, Afrika Kusini
JESHI la Polisi nchini Afrika Kusini limetoa dau la pauni milioni 8.5 kwa mtu yeyote atakayetoa taarifa za kukamatwa kwa watu waliomuua kipa wa timu ya soka ya Taifa ya Afrika Kusini, Bafana Bafana, Senzo Meyiwa.
Nahodha huyo wa klabu ya Orlando Pirates, alipigwa risasi kifuani, nyumbani kwa mpenzi wake, Kelly Khumalo.
Orlando Pirates, inashiriki michuano ya ligi kuu nchini Afrika Kusini na Senzo alikuwa mchezaji wa kutumainiwa wa kikosi hicho.
Mchezaji huyo alipigwa risasi juzi usiku katika eneo la Vosloorus, analoishi Kelly, lililoko maili 20 kutoka mji wa Johannesburg.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 27, aliuawa baada ya watu watatu kuvamia nyumba hiyo na kumpiga risasi kifuani kabla ya kutoweka.
Hivi karibuni, wapenzi hao walionekana katika picha ya pamoja iliyosambazwa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii na kuzua tafrani ndani ya familia yake.
Taarifa ya Jeshi la Polisi la Afrika Kusini ilisema kuwa, mchezaji huyo aliuawa saa chache baada ya picha yake kuonekana kwenye mitandap.
Khumalo, ambaye ni nyota wa muziki wa hip hop nchini Afrika Kusini, mpaka sasa yupo chini ya ulinzi wa Jeshi la Polisi kwa ajili ya uchunguzi wa tukio hilo.
"Watu wawili waliingia ndani ya nyumba ya Khumalo, walikuwa na silaha, mmoja alibaki nje na kumpira risasi Senzo eneo la kifuani.
"Watu hao wanasadikiwa kuwa ni majambazi kwa sababu waliiba baadhi ya vitu vya thamani, simu na fedha," ilisema taarifa ya polisi.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa, Senzo alikuwa katika harakati za kumuokoa Khumalo baada ya watu hao kumnyooshea bunduki mwanadada huyo kabla ya risasi walizotaka kumpiga kumfikia kipa huyo kifuani.
Siku moja kabla ya tukio hilo, kipa huyo aliiongoza Orlando Pirates katika mchezo wa ligi kuu ya Afrika Kusini dhidi ya Ajax Cape Town na kuibuka na ushindi wa mabao 4-1.
Kipa huyo amecheza mechi nne za mwisho za Bafana Bafana katika michuano ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika.
Senzo alizaliwa Septemba 24, 1987 katika mji wa Durban. Alianza kuichezea Orlando Pirates mwaka 2005 na timu ya taifa mwaka jana.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment