'
Tuesday, October 28, 2014
CHID BENZ ATINGA KIZIMBANI, AKOSA DHAMANA, APELEKWA SEGEREA
NA FURAHA OMARY
MSANII nyota wa muziki wa bongo fleva nchini, Rashid Makwaro (29),’Chid Benz’ amepandishwa kizimbani kwa tuhuma za kukutwa dawa za kulevya na kupelekwa mahabusu katika gereza la Segerea.
Chid Benz alifikishwa jana asubuhi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashitaka ya kukutwa na dawa za kulevya aina ya heroin zenye thamani y ash. 38,638, gramu 1.72 za bangi zikiwa na thamani ya sh. 1,072 na vitu vinavyotumika kuvutia na kunusia dawa hizo.
Msanii huyo alisomewa mashitaka hayo mnbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Warialwande Lema, ambaye kabla ya kuanza kusikiliza kesi hiyo aliamuru mshitakiwa huyo aondolewe ili akavae vizuri suruali kwa kuwa alikuwa amevaa ‘mlegezo’.
Chid Benz akiwa chini ya ulinzi wa poliisi aliingizwa katika chumba cha mahakama saa 7.38 mchana, huku akiwa amevaa tisheti ya bluu kwa ndani na shati la drafti la bluu vifungu vikiwa wazi karibu nusu.
Baada ya kuingizwa mbele ya Hakimu, Chid Benz alianza kufunga vifungo vya shati huku akiwa amevaa mlegezo, hali iliyomfanya hakimu aamuru kutolewa nje ili akavae vizuri suruali yake.
Msanii huyo alitolewa nje na kwenda kuvaa vizuri, ambapo aliporejea Wakili wa Serikali Mwanaamina Kombakono, akisaidiana na Mwendesha mashitaka Jackson Chidunda, walimsomea mashitaka.
Mwanaamina alidai Chid Benz alitenda makosa hayo, Oktoba 24, mwaka huu, katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, ulioko wilayani Ilala, Dar es Salaam.
Alidai siku hiyo, msanii huyo alikutwa isivyo halali na gramu 0.85 za dawa za kulevya aina ya heroin zenye thamani y ash. 38,638, gramu 1.72 za bangi zikiwa na thamani y ash. 1,720 na kijiko na kifuu cha nazi kitupu kinachotumika kwa ajili ya kuvutia na kunusia dawa hizo.
Chid Benz alikana mashitaka hayo, ambapo Wakili Mwanaamina alidai upelelezi haujakamilika na kwamba hawana pingamizi na dhamana juu ya mshitakiwa.
Hakimu Warialwande alitaja masharti ya dhamana ambayo ni sh. milioni moja na kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika ambao si walimu.
Hata hivyo, msanii huyo alishindwa kutimiza masharti hayo, hivyo kupelekwa rumande katika gereza la Segerea hadi Novemba 11, mwaka huu, kesi itakapotajwa. Msanii huyo aliondolewa mahakamani hapo kwa basi kubwa la kubebea mahabusu la Jeshi la Magereza.
Mahakamani hapo hakuonekana msanii hata moja kufuatilia kuhusu Chid Benz, zaidi ya familia yake.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment