'
Monday, October 6, 2014
SIMBA YABANWA NA STAND UNITED, YANGA YAIGAGADUA JKT RUVU
WAKATI timu kongwe ya soka nchini, Simba ikiendelea kusuasua katika michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Stand United, watani wao wa jadi Yanga wamezidi kupaa baada ya kuichapa JKT Ruvu mabao 2-1.
Simba ililazimishwa sare hiyo ya mabao na Stand United katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, matokeo yaliyopokewa kwa majonzi makubwa na mashabiki wa klabu hiyo.
Sare hiyo imeifanya Simba iwe imeambulia pointi tatu katika mechi tatu ilizocheza hadi sasa wakati Yanga imechupa nafasi za juu ikiwa na pointi sita katika mechi tatu.
Simba ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 35 kupitia kwa kiungo wake Shaaban Kisiga baada ya kupokea pasi kutoka kwa Emmanuel Okwi.
Bao hilo halikudumu kwa muda mrefu kwani dakika ya 45, Kheri Mohamed aliisawazishia Stand United baada ya kufanyika kwa shambulizi kali kwenye lango la Simba.
Nayo Yanga iliendelea kupaa nafasi za juu baada ya kuichapa JKT Ruvu mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Bao la kwanza la Yanga lilifungwa na beki Kevin Yondan kwa shuti kali la mbali, kufuatia kona iliyochongwa na kiungo Haruna Niyonzima.
Niyonzima aliiongezea Yanga bao la pili dakika ya 74 kwa mpira wa adhabu ndogo baada ya Genilson Jaja kuchezewa rafu nje kidogo ya eneo la hatari.
JKT Ruvu ilipata bao la kujifariji dakika ya 89 kupitia kwa mshambuliaji wake, Jabir Azizi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment