KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, October 8, 2014

LUNDENGA AMBWAGA PRASHANT PATEL MAHAKAMANI


NA FURAHA OMARY


MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemruhusu Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Lino International Agency, ambayo ni waandaaji wa mashindano ya Miss Tanzania, Hashim Lundenga, kuendelea na shindano hilo litakalofanyika Jumamosi, wiki hii, katika ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.

Hatua hiyo, inatokana na mahakama hiyo kutupilia mbali maombi yaliyowasilishwa na mshirika wa Lundenga, Prashant Patel ya kutoa zuio la muda la mashindano hayo.

Uamuzi huo, ulitolewa juzi jioni na Hakimu Mkazi Frank Moshi, baada ya kusikiliza maombi hayo yaliyowasilishwa na Patel kupitia Wakili wake Benjamin Mwakagamba.

“Mahakama baada ya kusikiliza maombi ya kutoa zuio la shindano hilo, imeona hakuna sababu za msingi zilizowasilishwa na mleta maombi (Patel) za kuweza kusimamisha shindano hilo,” alisema.

Hakimu Moshi alisema Patel aliwasilisha maombi hayo akidai kwamba kuna haki inakuikwa katika mkataba baina yake na Lundenga na bado zinaendelea kukiukwa.

Madai mengine ya Patel ni kwamba Lundenga amekuwa akiwasiliana na wafadhili na wadhamini wa shindano hilo bila ya kumshirikisha, hivyo alikuwa anaomba shindano hilo lisimamishwe kusubiri uamuzi wa mahakama.

“Hakukuwa na mashiko katika sababu za kutaka kutoa zuio na mahakama imejiuliza kama litatolewa linaweza kuleta athari kwa watu waliojitokeza, wadhamini na wanaotarajia kunufaika nalo kwa namna moja au nyingine kisa hawakujua kama kuna mgogoro.”

“Hata kama shindano litaendelea, madai ya msingi ya Patel yapo pale pale na hayaathiri. Shindano liendelee kama lilivyopangwa kwa kuwa kesi ya msingi inahusu fedha,” alisema Hakimu Moshi.

Patel alifungua kesi ya msingi mahakamani hapo dhidi ya Lundenga, Septemba 29, mwaka huu na baadae kuwasilisha maombi ya zuio la muda la mashindano hayo.

Baada ya kuwasilisha maombi hayo, Lundenga kwa kupitia wakili wake Audax Kahendaguza, aliwasilisha pingamizi la awali kupin ga kusimamishwa kwa shindano hilo. Mapema, jana mahakama hiyo ilisikiliza pingamizi la awali la Lundenga na kutolea uamuzi wa kulitupilia mbali.

Kutokana na kutupiliwa mbali kwa pingamizi hilo, mahakama hiyo ilisikiliza maombi ya Patel ya kutaka zuio la shindano hilo.

No comments:

Post a Comment