TIMU kongwe za soka nchini, Simba na Yanga zinashuka dimbani kesho kumenyana katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara, itakayopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Pambano hilo la watani wa jadi, linasubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka nchini kwa vile ndilo litakalomaliza ubishi wa timu ipi bora kati ya hizo msimu huu.
Simba itashuka dimbani huku mwenendo wake katika ligi hiyo ukiwa wa kusuasua baada ya kutoka sare katika mechi zote tatu za mwanzo.
Katika mechi yake ya kwanza, Simba ilitoka sare ya mabao 2-2 na Coastal Union, ikalazimishwa sare ya bao 1-1 na Polisi Moro kabla ya kulazimishwa sare nyingine ya bao 1-1 na Stand United ya Shinyanga.
Nayo Yanga ilianza vibaya ligi hiyo baada ya kuchapwa mabao 2-0 na Mtibwa Sugar, lakini ikazinduka katika mechi mbili zilizofuata baada ya kuichapa Prisons mabao 2-1 na kisha kuichapa JKT Ruvu mabao 2-1.
Katika mechi hiyo, Simba huenda ikawakosa makipa wake wawili, Ivo Mapunda na Hussein Sharifu 'Casillas' kutokana na kuwa majeruhi, hali inayomchanganya Kocha Mkuu wa timu hiyo, Patrick Phiri.
Iwapo makipa hao watashindwa kushuka dimbani, tegemeo pekee la Simba litakuwa kwa kipa wake chipukizi, Manyima Peter, ambaye ni mtoto wa kipa wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Peter Manyika.
Ivo alivunjika kidole cha mkono wiki mbili zilizopita wakati Sharifu ameumia kifundo cha mguu na atakuwa nje ya uwanja kwa miezi sita.
Hata hivyo, Phiri alisema taarifa za madaktari waliomtibu Ivo zimeeleza kuwa, huenda kipa huyo akawa fiti kabla ya mechi ya kesho.
Katika kujiandaa na mechi hiyo, Simba ilikwenda kuweka kambi ya siku 10 nchini Afrika Kusini na pia kucheza mechi tatu za kirafiki, ambapo ilichapwa mabao 2-0 na Jomo Cosmos, ilifungwa mabao 4-2 na Bidvest Wits na kutoka suluhu na Orlando Pirates.
Kwa upande wa Yanga, wachezaji wake Nadir Haroub 'Cannavaro' na Kevin Yondan, ambao walikuwa majeruhi, kwa sasa wapo fiti na wameanza mazoezi ya pamoja na wenzao.
Kocha Mkuu wa timu hiyo, Marcio Maximo amesema wachezaji wake wote wapo fiti na wana ari kubwa ya kushinda mchezo huo ili kulinda heshima yao.
Pambano hilo litachezeshwa na mwamuzi Israel Nkongo, ambaye Yanga iliandika barua kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ikilalamika kwamba haina imani naye na kutaka abadilishwe.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi ya TFF, Salum Umande alisema jana kuwa, wameamua kuyatupilia mbali maombi hayo ya Yanga kwa sababu hayana mashiko.
"Yanga waliandika barua ya kumlalamikia Mkongo katika mechi zao, lakini sisi tunachoangalia ni jinsi gani mwamuzi anatafsiri vyema sheria 17 za soka na katika hilo, Nkongo analimudu vyema,"alisema.
Hata hivyo, Umande alisema wameamua kumbadilisha mshika kibendera Ferdinand Chacha wa Mwanza, ambaye nafasi yake sasa itachukuliwa na Samuel Mpenzu kutoka Arusha. Mshika kibendera mwingine katika mechi hiyo atakuwa John Kanyenye kutoka Mbeya.
No comments:
Post a Comment