'
Tuesday, October 7, 2014
MASHIRIKISHO YA SANAA YAANDAA SEMINA KWA MAOFISA WA ULINZI NA USALAMA
Na Beatrice Lyimo, Maelezo
UMOJA wa Mashirikisho ya Sanaa Tanzania umeandaa semina itakayofanyika Jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 22-23 Oktoba mwaka huu kwa Maofisa wa vyombo vya ulinzi na Usalama pamoja na vyombo vya usimamizi wa sheria nchini ikiwa ni mkakati wa taasisi hiyo katika kukabiliana na tatizo la wizi wa kazi za wasanii nchini.
Hatua hiyo inakuja kufuatia Umoja huo kutoridhishwa na hatua stahiki ikiwemo adhabu zinazochuliwa na vyombo vyenye mamlaka ya kulinda na kutetea haki za wasanii nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu (Oktoba 6, 2014), Katibu wa Umoja huo, Godfrey Ndimbo alisema taasisi hiyo imekusudia kuendesha semina ya siku mbili kwa Maofisa wa taasisi za Jeshi la Polisi, Idara ya Uhamiaji na Mahakimu kwa malengo ya kutambua na kuthamini kazi za wasanii nchini.
“Tumeamua kushirikisha Maofisa wa Polisi, Maofisa wa Uhamiaji, na Mahakimu kwa kuwa tumebaini kuwa adhabu ya mtu ambaye anapatikana na hatia ya wizi wa kazi za msanii ni ndogo, tukiweza kuwashirikisha polisi na watu wa uhamiaji wataweza kujua tatizo lilivyo na jinsi ya kulikabili” alisema.
Aidha Ndimbo alisema semina hiyo, ambayo ni sehemu ya maandalizi ya siku ya Msanii Tanzania, inatarajia kushirikisha wasanii mbalimbali nchini, ambapo mada mbalimbali zinatarajia kuwasilishwa ikiwemo elimu kuhusu mafao ya uzeeni, matibabu kupitia bima za afya, Haki Miliki na HakiShiriki.
Aidha Ndimbo alizitaka taasisi mbalimbali kujitokeza katika kusaidia semina hiyo, kwa kuwa mafunzo hayo yamelenga katika kuwasaidia na kuwaendeleza wasanii wa Tanzania, hivyo kuungana na wasanii wengine ulimwenguni katika kusheherekea siku ya Msanii Duniani inayoadhimishwa tarehe 25. Oktoba kila mwaka ulimwenguni.
Akizungumzia kuhusu maadhimisho hayo, Ndimbo alisema katika maadhimisho hayo kutokuwepo na tuzo mbalimbali ikiwemo tuzo ya Humanitarian Award na Life Time Achievement ambazo zitatolewa kwa wasanii bora waliofanya kazi nzuri na kuthaminiwa na jamii.
“Tunaamini kwa tuzo hizi zitatoa changamoto kwa wasanii kujihusisha zaidi na jamii na kufanya kazi zao kwa ufanisi. Hii itawapa changamoto kufanya kazi bora na kusisitiza kauli mbiu ya mwaka huu isemayo Sanaa ni kazi” alisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment