'
Thursday, April 21, 2016
YANGA YATUPWA NJE MICHUANO YA KLABU BINGWA AFRIKA
MABINGWA wa soka wa Tanzania Bara, Yanga jana walitolewa katika michuano ya klabu bingwa Afrika baada ya kuchapwa mabao 2-1 na Al Ahly ya Misri.
Katika mechi hiyo ya marudiano ya raundi ya pili iliyochezwa mjini Cairo, Yanga ilikuwa ikihitaji ushindi ama sare ya zaidi ya mabao mawili ili iweze kusonga mbele.
Kutokana na kipigo hicho, Yanga imetolewa kwa jumla ya mabao 3-2, kufuatia timu hizo kutoka sare ya bao 1-1 katika mechi ya awali iliyochezwa mjini Dar es Salaam.
Mshambuliaji Abdalla Said ndiye aliyeisukuma Yanga nje ya mashindano hayo baada ya kuifungia Al Ahly bao la pili katika muda wa nyongeza.
Said alifunga bao hilo kwa kichwa kikali baada ya kupokea krosi kutoka kwa Walid Soliman. Kipa Dida wa Yanga alijaribu kuchupa kuokoa mpira huo, lakini aliishia kudaka hewa.
Al Ahly ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 52 kupitia kwa kiungo wake, Hossam Ghay, aliyeunganisha wavuni kwa kichwa kona ya Ahmed Fathi.
Yanga ilisawazisha bao hilo dakika ya 57 kupitia kwa mshambuliaji wa kimataifa wa Zimbabwe, Donald Ngoma, akimalizia krosi ya Juma Abdul.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment