'
Monday, April 25, 2016
PAPA WEMBA AFARIKI DUNIA AKIWA STEJINI
Jules Shungu Wembadio Pene Kikumba, ambaye wengi tulimfahamu kama Papa Wemba alizaliwa June 14, 1949, katika kijiji cha Lubefu Wilaya ya Sankuru huko Congo amefariki leo mapema baada ya kuanguka katikati ya show kwa kilichoelezwa ni kama kupata kifafa wakati akifanya onyesho katika tamasha la Femua katika jiji la Abidjan Ivory Coast.
Papa Wemba alikuwa mmoja ya wanamuziki wa kwanza kujiunga na bendi maarufu ya Zaiko mara baada ya kutengenezwa mwaka 1969, wakati huo alikuwa akijulikana kwa jina la Jules Presley Shungu Wembadio, bendi hii ilikuja kutambulika kama chuo cha wanamuziki wakubwa wa Kongo, na iliweza kupoporomosha vibao kama “Chouchouna” (Papa Wemba), “Eluzam” na ” Mbeya Mbeya” (Evoloko Lay Lay), “BP ya Munu” (Efonge Gina), “Mwana Wabi” na “Mizou” (Bimi Ombale) na wimbo “Zania” (Mavuela Somo).
Mwaka 1974 Shungu Wembadio , wakiwa na Evoloko Lay Lay, Mavuela Somo and Bozi Boziana wakaiacha Zaiko na kuanzisha kundi waliloliita Isifi Lokole.
Julai 1975, Shungu Wembadio ndipo alipojipa jina la Papa Wemba, kundi la Isifi liliishi mwaka mmoja na kuwa na wimbo mmoja tu uliouza sana “Amazone” utunzi wa Papa Wemba. Novemba 1975, Papa Wemba, Mavuela Somo na Bozi Boziana wakaihama Isifi na kuanzisha kundi la Yoka Lokole, ambalo nalo halikumaliza mwaka.
Kundi lilikufa pia kwa sababu Papa Wemba aliwekwa ndani kwa kudaiwa kuwa na mahusiano ya kingono na binti wa Jenerali wa jeshi. Baada ya mkasa huo ndipo Papa Wemba akaanzisha kundi la Viva la Musica, hiyo ilikuwa Februari 1977. Bendi ikaja na vibao kama “Mere Superieure,” “Mabele Mokonzi”, “Bokulaka,” “Princesse ya Sinza”.
Viva la Musica ilitoa wanamuziki wakali ambao waliendelea kufanya makubwa kama vile katika muziki wa Kongo. Wakali kama Fafa de Molokai, Debs Debaba, King Kester Emeneya, Koffi Olomide, Djuna Djanana, Dindo Yogo, Maray-Maray, Lidjo Kwempa, Reddy Amissi, Stino Mubi ni kati ya wanamuziki waliowahi kupitia Viva La Musica.
Koffi Olomide alipewa jina hilo na Papa wemba baada ya kutunga wimbo mmoja na Papa akafurahi na kumsifu na toka siku hiyo, Antoine Agbepa Koffi akajulikana kama Koffi Olomide .
Papa Wemba pia alijulikana kama muigizaji baada ya kucheza filamu ya La Vie est Belle na pia akaonekana tena kwenye filamu iliyoitwa Kinshasa Kids
Februari 18, 2003 Papa Wemba alikamatwa kwa kosa la kusaidia kuingiza wahamiaji haramu Ufaransa na akafungwa kwa miezi mitatu na nusu.
Mwenyewe alisema aliokoka wakati yuko jela na kuongelea hayo katika wimbo wake “Numéro d’écrou”, ambapo anasema Mungu alimtembelea gerezani.
Mwaka jana, Papa Wemba alifanya onyesho Bagamoyo kwenye tamasha la Karibu Music Festival. Mungu amlaze pema Papa Wemba.
IMETOLEWA KUTOKA BLOGU YA JOHN KITIME
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment