KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, April 4, 2016

YANGA YAIDUNDA KAGERA SUGAR, AZAM YALAZIMISHWA SARE NA TOTO AFRICANS


MABINGWA watetezi wa ligi kuu ya soka ya Tanzania Bara, Yanga jana waliendelea kuchanja mbuga baada ya kuichapa Kagera Sugar mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Ushindi huo umeiwezesha Yanga kuendelea kukamata nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo, ikiwa na pointi 53 baada ya kucheza mechi 22.

Simba bado inaongoza ligi hiyo, ikiwa na pointi 57 baada ya kucheza mechi 24 wakati Azam inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 51 kutokana na mechi 22 ilizocheza hadi sasa.

Kagera Sugar ilikuwa ya kwanza kupata bao lililofungwa na Mbaraka Yussuf baada ya kupokea pande safi kutoka kwa beki Salum Kanoni.

Donald Ngoma aliisawazishia Yanga dakika ya 26, baada ya kuunganisha wavuni kwa kichwa krosi kutoka kwa beki Juma Abdul. Timu hizo zilikwenda mapumziko zikiwa sare ya bao 1-1.

Kagera ilipata pigo dakika ya 47 baada ya beki wake, Shaaban Ibrahim kutolewa nje kwa kadi nyekundu na mwamuzi Erick Unoka kutoka Arusha, ikiwa ni kadi yake ya pili ya njano katika mchezo huo.

Mrundi Amissi Tambwe aliwainua vitini mashabiki wa Yanga dakika ya 62 baada ya kuifungiabao la pili, akimalizia krosi kutoka kwa Simon Msuva.

Bao la tatu la Yanga lilifungwa na beki wa kushoto, Haji Mwinyi baada ya kupokea pande kutoka kwa Msuva.

Katika mechi nyingine ya ligi hiyo iliyochezwa jana, Azam ililazimishwa kutoka sare ya bao 1-1 na Toto Africans kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.

Azam ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 23 lililofungwa na John Bocco kabla ya Waziri Juma kuisawazishia Toto dakika ya 40.

No comments:

Post a Comment