KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, April 18, 2016

SIMBA CHALI KWA TOTO AFRICAN

SI rahisi kuamini, lakini hivyo ndivyo ilivyotokea. Timu kongwe ya soka ya Simba jana ilipigwa mweleka wa bao 1-0 na Toto African ya Mwanza katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara,iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kipigo hicho kilipeleka majonzi makubwa kwa mashabiki wa Simba, ambao mara baada ya mchezo huo kumalizika, waliwafanyia vurugu viongozi na wachezaji wa klabu hiyo.

Mashabiki hao walisikika wakisema kuwa, wamechoshwa kuiona timu hiyo ikipokea vipigo mfululizo na hivyo kupoteza kabisa matumaini ya kutwaa ubingwa.

Kipigo hicho kilikuwa cha pili mfululizo kwa Simba. Wiki iliyopita, timu hiyo kongwe pia ilichapwa bao 1-0 na Coastal Union katika mechi ya Kombe la TFF.

Bao pekee na la ushindi la Toto African, lilifungwa na kiungo Waziri Junior dakika ya 20 kwa shuti la umbali wa mita 20 lililotinga moja kwa moja wavuni.

Katika mchezo wa leo, Simba ilicheza pungufu baada ya beki wake wa kulia, Hassan Ramadhani Kessy kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 47 kwa kumchezea rafu Edward Christopher wa Toto.

Mapema dakika ya 31, Kocha wa Simba, Mganda Jackson Mayanja aliondolewa kwenye benchi baada ya kumtolea maneno machafu refa Ahmed Simba wa Kagera.

Kwa matokeo hayo, Simba bado inashika nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi hiyo, ikiwa na pointi 57 baada ya kucheza 25, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 55 baada ya kucheza mechi 24. Yanga inaongoza kwa kuwa na pointi 59.

No comments:

Post a Comment