WAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya soka ya Kombe la Shirikisho, wameianza vyema baada ya kuichapa Esperance ya Tunisia mabao 2-1.
Katika mechi hiyo iliyochezwa jana kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, timu hizo zilikwenda mapumziko Esperance ikiwa mbele kwa bao 1-0.
Washambuliaji chipukizi Farid Mussa na Ramadhani Singano 'Messi' ndio walioibuka mashujaa wa Azam baada ya kuifungia mabao hayo mawili katika muda wa dakika mbili.
Kutokana na ushindi huo, Azam sasa inahitaji sare ya aina yoyote ili iweze kusonga mbele. Timu hizo zinatarajiwa kurudiana wiki mbili zijazo mjini Tunis.
Ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 33 lililofungwa na Haithem Jouini, aliyepachika mpira wavuni kwa kichwa baada ya kupokea krosi kutoka kwa Ilheb Mbaark.
Mabadiliko yaliyofanywa na Kocha Stewart Hall kipindi cha pili kwa kumtoa kiungo Kipre Balou na kumuingiza Frank Domayo yalirejesha uhai kwenye kikosi cha Azam.
Iliwachukua Azam hadi dakika ya 68 kupata bao la kusawazisha lililofungwa na Farid baada ya kutanguliziwa pasi na Messi.
Messi aliiongezea Azam bao la pili dakika ya 70 baada ya kupewa pasi na Farid.
No comments:
Post a Comment