'
Friday, April 8, 2016
NAPE AWAPA CHANGAMOTO WASANII
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Nape Nnauye (katikati) katika picha ya pamoja na waandishi wa habari wa Mkoa wa Geita baada ya kukutana nao jana mkoani hapo na kujadili fursa pamoja na changamoto mbalimbali zinazokabili sekta anazozisimamia. Kulia kwa Waziri ni Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe. Manzie Magochiena kulia ni Meneja wa Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) Kanda ya ziwa Eng. Lawi Odiero. Picha na: Genofeva Matemu – Maelezo, Geita
Na: Genofeva Matemu – Geita, Maelezo
Maafisa utamaduni nchini wametakiwa kushirikiana na wadau pamoja na kuandaa vikao vya mara kwa mara na wadau wa utamaduni wakiwemo wasanii ili kuweza kujenga ukaribu na kutoa elimu ya sanaa itakayosaidia kuboresha kazi za sanaa hivyo kutumia sanaa kutangaza maeneo ya utalii wa utamaduni yaliyopo nchini.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Nape Nnauye alipokutana na wadau wa sekta anazozisimamia pamoja na kutoa vitendea kazi kwa maafisa habari jana Mkoani Geita.
Mhe. Nnauye amesema kuwa kama maafisa utamaduni watakua karibu na wadau wa sanaa na utamaduni ujuzi wa tasnia ya sanaa na utamaduni utaongezeka kwa kujifunza kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine hivyo kukuza vipaji vya wasanii vitakavyotumika kutangaza maeneo ya utalii wa utamaduni na kuvutia watalii pamoja na wawekezaji.
Aidha Mhe. Nnauye ameitaka jamii kuheshimu kazi za sanaa na kuwathamini wasanii kwani serikali inampango wa kurasimisha kazi za sanaa hivyo kuifanya sanaa kuwa shughuli rasmi ya kiuchumi itakayowawezesha wawekezaji kuwekeza katika sanaa na kumfanya msanii apate kipato kizuri lakini pia kuiwezesha serikali kupata kipato kupitia tasnia ya sanaa na utamaduni.
Naye Mwenyekiti wa chama cha Waigizaji Mkoa wa Geita Bibi. Rosemery Michael amemuomba Mhe. Waziri kuhakikisha kuwa wasanii wanapata usajili na kuwa na uhalali wa kufanya kazi zao kwa kuhakikisha kuwa wasanii wanafuata sheria na taratibu zitakazowapa muongozo wa kufanya shughuli zao kwa ufanisi na weledi hivyo kuwaongezea kipato.
Bibi. Michael amesema kuwa tasnia ya sanaa inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo kutokuwa na chuo cha sanaa mikoani, wasanii kutokua na elimu ya sanaa itakayowajengea uwezo wa kujikwamua kiuchumi, wasanii kufanya kazi kiholela, pamoja na uhaba wa uwekezaji katika tasnia ya sanaa.
Aidha Katibu wa Chama cha waigizaji Mkoa wa Geita Bw. Kangeta Ismaili ameomba mfuko wa maendeleo ya vijana kutambua vikundi vya wasanii na kuvifikia vikundi hivyo kwa kuwapa mikopo ambayo itawawezesha kuboresha kazi za sanaa na kuwainua wasanii kiuchumi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment