'
Monday, April 11, 2016
KANU AAHIDI KUSAIDIA KUINUA SOKA YA TANZANIA
Na Eleuteri Mangi-MAELEZO
BALOZI wa Star Times barani Afrika, Nwankwo Kanu, ameahidi kusaidia kuinua kiwango cha soka nchini kwa kutoa mafunzo kwa vijana.
Kanu, alisema hayo mwishoni mwa wiki, baada ya kupokea zawadi ya jezi ya timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, yenye jina lake kutoka kwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Selestine Mwesigwa.
Mwanasoka huyo wa zamani wa kimataifa wa Nigeria, alisema amekuja nchini kwa mwaliko wa Star Times, lakini amepanga kuja tena kwa shughuli zake binafsi za kimichezo.
Kanu, ambaye aliwahi kung'ara kisoka alipokuwa klabu za Ajax Amsterdam ya Uholanzi, Inter Milan ya Italia, Arsenal, West Bromwich na Portsmouth za England, alisema amefurahishwa na mapokezi aliyoyapata wakati wa ziara yake hapa nchini.
Kutokana na mapokezi hayo, Kanu alisema anaamini mchango wake katika soka ya Tanzania unahitajika.
“Mustakabali wa mpira wa miguu wa Tanzania utakuwa mkubwa kama Watanzania watapenda kufuatilia masuala ya mpira wa miguu kupitia ligi tofauti tofauti. Kadri unavyoangalia michezo mbalimbali ya kimataifa, ndivyo unavyozidi kujifunza,” alisema Kanu.
Kwa upande wake, Mwesigwa aliishukuru Star Times Tanzania kwa kuthamini soka kwa kumleta nchini mchezaji nguli wa kimataifa wa Nigeria, Kanu.
Mwesiga, aliyasema hayo mwishoni mwa wiki, jijini Dar es Salaam, kwenye hafla ya chakula cha jioni, kilichoandaliwa na Kampuni ya StarTimes, kwa lengo la kumkaribisha Kanu.
“Kupitia StarTimes, tutaboresha mpira wetu kwa kuangalia ligi mbalimbali za mataifa ya Ujerumani, Italia na Ufaransa,” alisema Mwesigwa.
Kanu, alifanyiwa upasuaji wa moyo mwaka 1996 na ndipo alipoamua kufungua taasisi yake ya moyo inayoitwa 'The Kanu Heart Foundation.'
Taasisi hiyo iliyoko nchini Nigeria, ambako ndiko alikozaliwa, aliianzisha kwa madhumuni ya kuwasaidia wagonjwa wenye matatizo ya moyo na ameahidi kushirikiana na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete katika masuala mbalimbali ya kitabibu.
Wakati huo huo, Kanu ametembelea na kushiriki kutoa mafunzo kwa watoto wa kituo cha Jakaya Mrisho Kikwete Youth Park cha jijini Dar es Salaam.
Akiwa kwenye kituo hicho, Kanu alielezea kufurahishwa kwake kuona watoto hao watoto wameandaliwa mazingira mazuri kwa ajili ya michezo mbalimbali, kwa kuwa sio wengi wanaopata fursa hiyo.
“Wakati mimi ninaanza kucheza mpira, hakukuwa na kituo kizuri kama hiki wala jezi, viatu na walimu wazuri mlio nao sasa. Hii ni fursa ya kipekee kwenu nyinyi kuweza kuonyesha juhudi za kujifunza ili mje kuwa kama mimi siku za mbeleni.
"Leo mimi nimekuwa maarufu ni kwa sababu nilikuwa na nidhamu, bidii, dhamira na kuwasikiliza walimu wangu walipokuwa wananifundisha. Hatimaye leo hii nina mafanikio makubwa, ninaishi maisha mazuri, wazazi wangu pia wanaishi mahali pazuri, wanasafiri na kupata wanachokitaka kwa sababu tu ya mimi kufanikiwa,"Kanu aliwaambia watoto hao.
Aliwataka watoto wa kituo hicho kuonyesha bidii, utii na dhamira ya dhati kwa kila wanachokifanya.
"Ningependa kuwashauri wadogo zangu kuwa popote utakapokwenda duniani kwenye mchezo wa soka, viwanja na mipira inayotumika ni hii hii wala hakuna tofauti yoyote.
"Hivyo sioni kama kuna kitu cha kuwazuia na nyinyi msifanikiwe. Kama nilivyowaambia awali, bidii, nidhamu, dhamira na utii kwa walimu wenu ndio msingi wa mafanikio ya mwanasoka yeyote yule duniani. Nawatakia kila la kheri na siku nyingine nikija Tanzania naahidi kuwatembelea tena,” aliwasisitizia vijana hao.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment