'
Sunday, April 3, 2016
SERENGETI BOYS YAIFANYIA KWELI MISRI
KIKOSI cha timu ya soka ya Taifa ya Vijana wa chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys, jana kiliibuka wababe dhidi ya vijana wa umri huo wa Misri.
Katika mechi hiyo ya kirafiki ya kimataifa iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Serengeti Boys ilikwenda mapumziko ikiwa mbele kwa bao 1-0.
Mshambuliaji Benedicto aliifungia Serengeti Boys bao la kuongoza dakika ya 15 baada ya kufumua shuti kali la mbali lililowapita mabeki na kipa wa Misri.
Katika mechi hiyo, vijana wa Serengeti Boys walionyesha uwezo mkubwa wa kutandaza kabumbu, lakini walichokikosa ni kucheza soka ya kufundishwa. Karibu kila mchezaji alionyesha uwezo wake binafsi, isipokuwa mara chache waligongeana vizuri.
Mabadiliko yaliyofanywa na Misri katika kipindi cha pili yaliipa uhai timu hiyo na kuongeza kasi ya mchezo kabla ya kusawazisha dakika ya 85 kwa bao lililofungwa na Diah Waheed.
Bao hilo halikuwakatisha tamaa vijana wa Serengeti Boys, ambao walifanya mashambulizi kadhaa kwenye lango la Misri, lakini walishindwa kuzifumania nyavu.
Ikiwa imesalia dakika moja pambano hilo kumalizika, Ally Hussein aliwainua vitini mashabiki wachache waliofika uwanjani baada ya kuifungia Serengeti Boys bao la pili.
Timu mbili hizo zinatarajiwa kurudiana tena Jumanne kwenye uwanja huo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment