'
Sunday, April 27, 2014
WACHINA KUUKARABATI UWANJA WA MAO TSE TUNG
Balozi Mdogo wa Jamuhuri ya Watu wa China aliyepo Zanzibar Bwana Xie Yunliang akiwasilisha agizo la Serikali yake kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi la kuridhia na kukubali kusaidia Ujenzi wa uwanja wa Michezo wa Mau Tse Tung uliopo Mtaa wa Mperani - Kikwajuni Mjini Zanzibar
Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China imeridhia na kukubali kugharamia ujenzi wa Kiwanja cha michezo kilichopewa jina na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar la Mau Tse Tung kilichopo miperani Kikwajuni Mjini Zanzibar.
Kauli hiyo imetolewa na Balozi Mdogo wa Jamuhuri ya Watu wa China aliyepo Zanzibar Bw. Xie Yunliang wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo katika Ofisi yake iliyomo ndani ya Jengo la Msekwa Bungeni Mjini Dodoma.
Balozi Xie Junliang alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Timu ya wataalamu wa China inatarajiwa kukifanyia utafiti na uchunguzi kiwanja hicho baadaye mwaka huu sambamba na utiwaji saini Makubaliano ya ujenzi wa kiwanja hicho unaotarajiwa kufanyika mapema mwaka ujao.
Alisema ujenzi wa uwanja huo uliopewa heshima ya Jina la Kiongozi muasisi wa Taifa la China Marehemu Mao Tse Tung utajumuisha kiwanja cha mchezo wa soka pamoja na michezo mengine ya ndani mfano mchezo wa Table Tennis.
“ Tunatarajia ujeni wa kiwanja cha Mao utakapokamilika utakuwa na uwezo wa kuhudumia wanamichezo wa michezo tofauti ukiwemo ule unaopendwa zaidi wa soka “. Alisema Bwana Xie Junliang.
Balozi Mdogo wa China aliyepo Zanzibar alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba uhusiano wa kidugu uliopo kati ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla pamoja na China unastahiki kuenziwa zaidi.
Alimuhakikishia Balozi Seif kwamba Jamuhuri ya Watu wa China itaendelea kuiunga mkono Zanzibar na Tanzania kwa ujumla katika harakati zake za kujikwamua kiuchumi.
Alisema matengenezo makubwa ya ujenzi wa Hospitali ya Abdulla Mzee iliyopo Mkoani Kisiwani Pemba, ujenzi wa maegesho ya ndege katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Zanzibar pamoja na matayarisho wa matengenezo ya chumba cha wagonjwa mahututi { ICU } mwezi Juni mwaka huu katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja ni miongoni mwa uthibitisho wa uhusiano wa pande hizo mbili.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameipongeza Jamuhuri ya Watu wa China kwa moyo wake wa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar na Tanzania kwa ujumla katika miradi ya Kiuchumi na Maendeleo.
Balozi Seif alisema mchango wa Serikali ya China kwa Zanzibar umesaidia kuiwawezesha asilimia kubwa ya Jamii Zanzibar kustawika Kijamii na hata kiuchumi kupitia miundo mbinu iliyowekwa na Serikali kwa msaada wa Nchi hiyo rafiki.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitolea mfano msaada mkubwa uliotolewa na China katika ujenzi wa skuli za Wilaya za Sekondari katika Wilaya zote za Unguja na Pemba.
Alisema mradi huo mkubwa wa sekta ya Elimu umekuja kufuatia ongezeko kubwa la idadi wa wanafunzi wanaofanikiwa kujiunga na masomo ya Sekondari katika maeneo tofauti ya Zanzibar.
“ Kutokana na ongezeko kubwa la wanafunzi hasa eneo la Wilaya ya Magharibi katika Kisiwa cha Unguja tumelishuhudia hivi karibuni katika skuli ya Kijitoupele na Serikali kupitia Wizara ya Elimu tunaliangalia tatizo hilo kwa mtazamo wa kujenga skuli mpya katika Mtaa wa Pangawe “. Alisema Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliipongeza China kupitia Balozi wake huyo kwa mchango wake mkubwa katika Nyanja ya Elimu mchango ambao tayari watoto wa Zanzibar wanaendelea kufaidika nao.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment