'
Sunday, April 13, 2014
AZAM YAIVUA UBINGWA YANGA, SIMBA YAPIGWA NA ASHANTI
AZAM jana ilifanikiwa kuweka rekodi ya kutwaa ubingwa wa ligi kuu ya Tanzania Bara kwa mara ya kwanza baada ya kuichapa Mbeya City mabao 2-1 katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
Azam imetwaa ubingwa huo huku ikiwa na mechi moja mkononi baada ya kufikisha pointi 59, ambazo haziwezi kufikiwa na mabingwa wa mwaka jana, Yanga ambayo jana iliichapa JKT Oljoro mabao 2-1 mjini Arusha.
Yanga imesaliwa na mechi moja dhidi ya Simba itakayochezwa Aprili 19 mwaka huu mjini Dar es Salaam na iwapo itashinda, itafikisha pointi 58.
Iliwachukua Azam dakika 44 kuhesabu bao la kwanza lililofungwa na Gaudence Mwaikimba baada ya kutokea piga nikupige kwenye lango la Mbeya City.
Mbeya City ilisawazisha dakika ya 70 kwa bao lililofungwa na Mwigane Yeya kwa tiktak.
Wakati mashabiki wakidhani mechi hiyo ingemalizika kwa sare, John Bocco alibadili matokeo dakika ya 84 baada ya kuifungia Azam bao la pili.
Pambano kati ya Yanga na JKT Oljoro lilikuwa na ushindani mkali kutokana na timu hizo mbili kucheza kwa kukamiana.
JKT Oljoro ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 68 lililofungwa na Jacob Masawe baada ya kupokea pasi kutoka kwa Shija Mkina.
Yanga ilisawazisha dakika ya 75 baada ya Rajabu Zahir, aliyeingia badala ya Ibrahim Job kufunga bao.
Bao la pili na la ushindi la Yanga lilifungwa na Mrisho Ngasa dakika ya 71 baada ya kupokea krosi kutoka kwa Simon Msuva.
Wakati huo huo, timu kongwe ya soka nchini, Simba jana ilipigwa mweleka wa bao 1-0 na Ashanti katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Bao pekee na la ushindi la Ashanti lilifungwa na Mohamed Nampaka dakika ya 17 baada ya kupokea pasi kutoka kwa Hassan Kabunda.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment