Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF imekutana Machi 30 mwaka huu kujadili utekelezaji wa maagizo ya TFF kwa wanachama wake kurekebisha Katiba zao ili ziendane na Katiba ya TFF pamoja na ile ya FIFA kabla ya Machi 30 mwaka huu.
Vyama vya mikoa Lindi na Dar es Salaam na Chama cha Mpira wa Miguu cha Wanawake (TWFA) viliomba kuongezewa muda wakati vingine vimeomba Katiba mama kama angalizo lao la mabadiliko hayo. Klabu ya Simba Sports ndiye mwanachama pekee aliyewasilisha mabadiliko ya Katiba. TFF inawapongeza viongozi na wanachama wa klabu hiyo kwa kufanya mkutano wao kwa utulivu.
Kamati itatangaza nyongeza ya muda wa kufanya mabadiliko hayo baada ya kuviandalia vyama vya mikoa na vyama shiriki katiba mfano kwa ajili ya kurahisisha shughuli hiyo.
Baada ya kupitia uamuzi wa wanachama wa Simba S.C. Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji imeamua ifuatavyo:
(i) Kwa kuwa pendekezo la wanachama wa Simba kubadili kipengele na 26 kuhusu sifa za mgombea kinapingana na kipengele na 29 (4) cha Katiba ya TFF, hivyo basi Kamati imeagiza kipengele cha Katiba ya Simba kibaki vilevile bila kubadilishwa.
(ii) Vipengele vingine vyote vimepitishwa na vitapelekwa kwa Msajili wa Klabu na Vyama vya Michezo kwa ajili ya kusajiliwa.
(iii) Mchakato wa uchaguzi wa Klabu ya Simba uendelee kama ulivyopangwa wakizingatia uamuzi huu wa Kamati. TFF inaitakia Klabu ya Simba uchaguzi mwema.
Pia Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji imeshauri TFF kuwasiliana na FIFA kupata mwongozo kuhusu katazo la watu wenye rekodi ya kifungo kugombea.
TFF imepokea ushauri huo na itaufanyia kazi na kama kuna mabadiliko yoyote kiutaratibu yataanzia katika Katiba ya TFF kupitia Mkutano Mkuu.
No comments:
Post a Comment