'
Thursday, April 10, 2014
YANGA RAHA TUPU
MAMIA ya mashabiki wa Yanga jana walitoka uwanjani roho kwatu baada ya kuishuhudia timu yao ikipata ushindiwa mabao 2-1 dhidi ya Kagera Sugar.
Katika mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Yanga ilicheza kwa kasi kubwa na kuweza kuvuna pointi zote tatu kutoka kwa wapinzani wao.
Kutokana na ushindi huo, Yanga imefikisha pointi 52 na iko nafasi ya pili, nyuma ya vinara Azam wenye pointi 53. Mechi ya Azam na Ruvu Shooting haikuchezwa jana kutokana na mvua kubwa kunyesha mkoani Pwani.
Mechi hiyo, ambayo itaonyesha mustakabali wa timu ipi itakayotwaa ubingwa wa ligi kuu msimu huu, sasa itachezwa leo kwenye uwanja wa Mabatini ulioko Mlandizi.
Yanga sasa imebakiwa na mechi mbili dhidi ya JKT Oljoro itakayochezwa Aprili 13 mjini Arusha kabla ya kuvaana na watani wao Simba katika mechi ya mwisho itakayopigwa Aprili 19 mwaka huu.
Kwa upande wa Azam, baada ya mechi ya leo, itasaliwa na mechi zingine mbili dhidi ya Mbeya City itakayochezwa mjini Mbeya kabla ya kuvaana na JKT Ruvu.
Yanga ilihesabu bao lake la kwanza dakika ya tatu kupitia kwa mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda, Hamisi Kiiza, kufuatia kazi nzuri iliyofanywa na Simon Msuva.
Bao la pili la Yanga lilifungwa na Didier Kavumbagu dakika ya 34 kwa shuti kali baada ya kupokea pasi kutoka kwa Msuva.
Kagera ilipata bao la kujifariji dakika ya 62 kupitia kwa mshambuliaji wake, Daudi Jumanne baada ya beki Oscar Joshua kumrejeshea mpira dhaifu kipa wake, Deogratius Munishi 'Dida.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment