KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, April 27, 2014

CECAFA YAANZISHA MICHUANO MIPYA, INAITWA KOMBE LA NILE, YANGA KUIWAKALISHA TANZANIA



BARAZA la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), limeanzisha mashindano mapya yatakayojulikana kwa jina la Nile Basin Cup.

Taarifa iliyotolewa na baraza hilo jana imeeleza kuwa, timu zitakazoshiriki kwenye michuano hiyo ni zile zilizoshika nafasi za pili katika ligi za kila nchi zilizo wanachama.

Michuano hiyo imepangwa kuanza Mei 20 hadi Juni 5 mwaka huu nchini Sudam na tayari wenyeji kwa kushirikiana na CECAFA wamepata wadhamini watakaogharamia usafiri wa kwenda na kurudi kwa timu zote, malazi, usafiri wa ndani na zawadi za fedha.

Katika michuano hiyo, Tanzania itawakilishwa na Yanga, ambayo imeshika nafasi ya pili katika michuano ya mwaka huu ya ligi kuu ya Tanzania Bara.

Mbali na michuano hiyo, CECAFA pia imeamua kuanzisha mashindano ya vijana wa chini ya umri wa miaka 23 inayotarajiwa kufanyika Septemba mwaka huu nchini Sudan.

Taarifa hiyo imesema lengo la michuano hiyo ni kuzipa maandalizi nchi wanachama kwa ajili ya michezo ya Olimpiki ya mwaka 2016. Imesema serikali ya Sudan imejitolea kudhamini michuano hiyo.

Katika hatua nyingine, michuano ya mwaka huu ya Kombe la Kagame, imepangwa kufanyika Agosti nchini Rwanda.

Tayari Rais Paul Kagame wa Rwanda ameshajitolea kudhamini michuano hiyo kwa kutoa dola 60,000 za Marekani kwa ajili ya fedha za zawadi kwa washindi.

Wakati Kombe la Kagame litachezwa Rwanda, michuano ya Kombe la Chalenji imepangwa kufanyika kati ya Novemba na Desemba mwaka huu nchini Ethiopia.

Ujumbe wa CECAFA unatarajiwa kwenda Ethiopia baada ya kumalizika kwa fainali za Kombe la Dunia kwa ajili ya kufanya maandalizi ya mwisho na kutafuta wadhamini.

Wakati huo huo, Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA) limeandaa semina ya mawasiliano kwa nchi wanachama wa CECAFA itakayofanyika Aprili 30 hadi Mei 2 mwaka huu mjini Dar es Salaam.

Semina hiyo itahudhuriwa na maofisa wa habari, wakurugenzi, wenyeviti wa vyama vya mikoa, makatibu wakuu na vyama vyote vilivyo wanachama wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Semina hiyo inatarajiwa kufunguliwa na Katibu Mkuu wa FIFA, Jerome Valcke, anayetarajiwa kuwasili nchini hivi karibuni.

Katika hatua nyingine, CECAFA imeingia mkataba mpya wa miaka minne na kituo cha televisheni cha Supersport cha Afrika Kusini. Mkataba huo umeanza 2014 na utamalizika 2017.

Kwa mujibu wa mkataba huo, Supersport itaonyesha live michuano yote inayoandaliwa na CECAFA.

No comments:

Post a Comment