'
Wednesday, August 3, 2011
Wasanii wawashukia wasambazaji wa kazi zao
WASANII wa kazi mbalimbali za sanaa nchini wamewatupia lawama wasambazaji wa kazi zao kwa madai kuwa, wamevuruga mfumo wa usambazaji.
Wakizungumza kupitia programu ya kila wiki ya Jukwaa la Sanaa kwenye ofisi za Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) mwanzoni mwa wiki hii, wasanii hao walisema wasambazaji wa zamani wameshindwa kuhimili mfumo wa sasa.
Walizitaja sababu zilizosababisha kuvurugika kwa mfumo huo kuwa ni pamoja na wasambazaji hao kushusha bei za CD/DVD hadi shilingi elfu moja na pia kuwashusha thamani wasanii chipukizi.
Sababu zingine zilizotajwa na wasanii hao ni kuwabana wasanii wenye majina makubwa washirikiane na wale chipukizi na pia ununuaji wa hakimiliki za wasanii kinyume cha sheria.
Kwa mujibu wa wasanii hao, sababu nyingine ni kutokuwepo kwa mfumo mzuri wa kugawa kazi za wasanii kwenye madaraja.
“Leo hii, CD zinauzwa mtaani kwa shilingi elfu moja, hivi kweli kazi za wasanii wa Tanzania zimefikia kiwango cha kuuzwa kwa kiasi hicho cha pesa? Ni msambazaji gani ataweza kuhimili ushindani wakati kuna kampuni imeshusha thamani ya kazi za wasanii kwa kiwango hicho?” Alihoji Michael Sangu, ambaye ni msanii wa filamu.
Akijibu hoja za wasanii hao, Meneja wa Uzalishaji wa Kampuni ya Steps Entertainment, Kambarage Ignatus alisema, kampuni yake inafanya biashara, hivyo inajikita zaidi kutafuta faida.
Ignatus alisema kwa kuzingatia ukweli huo, kampuni yake inatilia mkazo kusambaza kazi zenye ubora na kuuzika.
Alikanusha madai kuwa, kampuni yake imekuwa ikiwabana wasanii maarufu ili wasifanyekazi na wale wanaochipukia na kusisitiza kuwa, kazi yoyote ya msanii ni makubaliano kati yake na kampuni.
“Hatuwezi kusambaza kila kazi ya msanii, wasanii ni wengi sana, isipokuwa tunalenga zile zenye ubora na kuuzika,”alisisitiza.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment