Mechi ya Ngao ya Jamii (Community Shield) kufungua msimu mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom kati ya mabingwa watetezi Yanga na Makamu Bingwa Simba itachezwa usiku (Agosti 17 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Uamuzi wa mechi hiyo kuchezwa kuanzia saa 2.00 usiku umetokana na sababu kadhaa, kubwa zikiwa mbili; Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan na pia Agosti 17 mwaka huu kuwa ni siku ya kazi.
Pambano hilo litatanguliwa na mechi ya vikosi vya pili (U20) vya timu hizo ambayo yenyewe itaanza saa 10.30 jioni. Mechi ya Ngao ya Jamii baada ya dakika 90 kama mshindi hatapatikana, zitaongezwa dakika 30. Katika muda huo nao kama mshindi atakuwa bado hajapatikana, itatumika mikwaju ya penalti.
Mechi hiyo imepata mwekezaji (Bigbon) na hivi sasa wadau wake wakuu- Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na klabu husika ziko katika mazungumzo ya mwisho mwekezaji huyo.
Kwa redio ambazo zinataka kutangaza mechi hiyo moja kwa moja zinatakiwa kuwasiliana na Idara ya Habari na Mawasiliano ya TFF ili kupewa masharti ya kufanya hivyo.
Pia unafanyika utaratibu wa kuuzwa futari uwanjani mara baada ya mechi ya vikosi vya pili ili kuwawezesha washabiki waliofunga kutohangaika kutafuta sehemu ya kufuturu.
No comments:
Post a Comment