'
Thursday, August 11, 2011
Timbe kuifumua Yanga
KOCHA Mkuu wa Yanga, Sam Timbe amesema atakifumua na kukisuka upya kikosi chake kabla ya pambano lao la kuwania Ngao ya Hisani dhidi ya Simba litakalochezwa Agosti 17 mwaka huu.
Timbe alisema hayo jana muda mfupi mara baada ya timu hiyo kuwasili kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere mjini Dar es Salaam ikitokea Sudan.
Kocha huyo kutoka Uganda alisema, amefikia uamuzi huo baada ya kubaini kasoro kadhaa za kiufundi kwa baadhi ya wachezaji wake, baada ya kucheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya El-Merreikh ya Sudan.
Katika mechi hizo zilizochezwa juzi na Jumapili iliyopita, Yanga ilichapwa mabao 3-1 kila mechi na El-Merreikh.
Timbe alisema ataanza kukifumua kikosi hicho katika mazoezi yatakayofanyika leo kwenye uwanja wa Kaunda uliopo Jangwani mjini Dar es Salaam.
Akizungumzia vipigo hivyo, Timbe alisema vilitokana na kiwango cha juu kilichoonyeshwa na wapinzani wao, ambao aliwaelezea kuwa wapo juu kisoka ikilinganishwa na Yanga.
“Hatukucheza vizuri mechi ya kwanza kwa sababu tulishindwa kufanya mazoezi na kuzoea hali ya hewa ya huko. Tulicheza mechi siku moja baada ya kuwasili Sudan, hali hiyo ilituathiri,”alisema.
“Lakini kikubwa ni kwamba, wachezaji wangu hawakuwa vizuri kisaikolojia kutokana na matatizo mbalimbali yaliyojitokeza kwa timu yetu, lakini tutayarekebisha matatizo hayo,”aliongeza bila kubainisha matatizo hayo.
Pamoja na kupata vipigo hivyo, Timbe aliwasifu wachezaji wake kwa kuonyesha kiwango cha juu kisoka na kuongeza kuwa, mapungufu yaliyojitokeza katika mechi hizo, atayafanyiakazi.
Akizungumzia pambano lao dhidi ya Simba, kocha huyo alisema atatumia siku chache zilizosalia kuiandaa vyema timu yake kukabiliana na wapinzani wao hao wa jadi na kusisitiza kuwa, ushindi ni muhimu.
Wakati huo huo, Yanga juzi ilipata kipigo kingine cha mabao 3-1 kutoka kwa El-Merreikh ya Sudan katika mechi ya kirafiki iliyochezwa mjini Khartoum.
Kipigo hicho kilikuwa cha pili kwa Yanga kutoka kwa El-Merreikh katika ziara yake ya mechi za kirafiki nchini Sudan kwa ajili ya maandalizi ya michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara.
Katika mechi ya awali kati ya timu hizo, iliyochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita, Yanga ilipata kichapo cha idadi hiyo ya mabao kutoka kwa El-Merreikh.
Awali, Yanga ilikuwa icheze mechi nyingine ya kirafiki dhidi ya El-Hilal, lakini pambano hilo lilifutwa dakika za mwisho.
Kama ilivyokuwa katika mechi ya kwanza, Yanga ilionyesha uhai katika kipindi cha kwanza, lakini ilionekana kuzidiwa kipindi cha pili, ambapo wenyeji walitawala mchezo.
Yanga ilikuwa ya kwanza kupata bao kipindi cha kwanza, lililofungwa na mshambuliaji wake wa kimataifa kutoka Ghana, Kenneth Asamoah.
Mabingwa hao wa Tanzania Bara walipata pigo kipindi cha pili baada ya kipa wake, Yaw Berko kuumia na kuingia Saidi Mohamed.
Kutoka kwa Berko kulitoa mwanya kwa wenyeji kufunga mabao hayo matatu na hatimaye kutoka uwanjani na ushindi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment