KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, August 3, 2011

SIMBA, YANGA VICHEKO TUPU

MKURUGENZI wa Masoko wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), David Minja (wa pili kushoto), akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa klabu za Simba, Yanga na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), mara baada ya utiaji saini wa mikataba mipya kati ya kampuni hiyo na klabu hizo. Kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange 'Kaburu', wa tatu kushoto ni Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah na kulia ni Mwenyekiti wa Yanga, Lloyd Nchunga. (Na mpiga picha wetu).


NEEMA imezishukia klabu za Simba na Yanga baada ya Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia yake ya Kilimanjaro, kuingia mkataba wa udhamini wa miaka minne na klabu hizo.
Katika mkataba huo, uliotiwa saini jana kwenye hoteli ya Double Tree mjini Dar es Salaam, TBL imeongeza fedha za mishahara kwa wachezaji kutoka sh. milioni 16 hadi sh. milioni 25 kila mwezi.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini mikataba hiyo, Mkurugenzi wa Masoko wa TBL, David Minja alisema, kampuni hiyo pia itatoa basi moja kwa kila klabu lenye uwezo wa kubeba abiria 54 na pia kugharamia mikutano ya wanachama ya kila mwaka.
Minja alisema kampuni hiyo pia itatoa sh. milioni 20 kwa kila klabu kwa ajili ya kugharamia matamasha ya ‘Simba Day’ na ‘Yanga Day’ kila mwaka pamoja na kutoa vifaa vya michezo vyenye thamani ya sh. 35 kwa kila msimu wa ligi.
Mkurugenzi huyo alisema, TBL pia imeongeza viwango vya zawadi kwa timu hizo, ambapo ile itakayotwaa ubingwa wa ligi kuu, itazawadiwa sh. milioni 25 na ile itakayotwaa nafasi ya pili itapata sh. milioni 15.
Minja alisema, mkataba huo wenye thamani ya zaidi ya sh. bilioni tano, unatarajiwa umeanza Agosti 8 mwaka huu na unatarajiwa kumalizika Julai 31, 2016.
Katika hafla hiyo, Simba iliwakilishwa na Makamu Mwenyekiti, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ wakati Yanga iliwakilishwa na Mwenyekiti wake, Lloyd Nchunga. Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), liliwakilishwa na Katibu Mkuu wake, Angetile Osiah.
Awali, TBL iliingia mkataba wa udhamini na klabu hizo kwa miaka mitatu kuanzia mwaka 2008.
“Tunazishukuru klabu zote mbili kwa kukubali kushirikiana na Kilimanjaro kwa awamu nyingine tena,”alisema Minja na kuzitaka klabu hizo kuheshimu mikataba hiyo.
Kwa upande wake, Nchunga alisema TBL imekuwa mfano wa kuigwa kwa maendeleo ya soka nchini na kwa vile inatumia fedha nyingi kuzifanya klabu hizo zifanye vizuri katika michuano mbalimbali.
Naye Kaburu aliishukuru kampuni hiyo kwa kuendelea kuidhamini klabu yake na kuongeza kuwa, watautumia udhamini huo kuiletea mafanikio makubwa zaidi Simba.

No comments:

Post a Comment