KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, August 11, 2011

Kabeya awaponda wanaojiita 'wazee wa masauti'


MWANAMUZIKI mkongwe nchini, Kabeya Badu amewaponda wanamuziki wanaojiita ‘wazee wa masauti’ kwa madai kuwa uwezo wao kimuziki ni mdogo.
Akihojiwa katika kipindi cha Mwanamuziki Wetu cha TBC FM mwishoni mwa wiki iliyopita, Kabeya alisema sifa wanazojipa wanamuziki hao hazilingani na uwezo wao na hawapendi kujifunza.
Kabeya alisema tatizo hilo lipo kwa wanamuziki wengi nchini hivi sasa na linatokana na kutopenda kwao kupata ushauri na maelekezo kutoka kwa wakongwe wa fani hiyo.
Hata hivyo, mwanamuziki huyo kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo alisema, zipo baadhi ya bendi nchini, hasa zile kongwe, ambazo zinapiga muziki wenye mvuto na unaoweza kupendwa kimataifa.
Alisema baadhi ya bendi hizo, kama vile Msondo Ngoma na Mlimani Park Orchestra, zinaweza kupata mashabiki kokote barani Afrika kwa vile zinapiga muziki wa kuvutia.
“Wakati nakuja nchini, nilikuwa nikipenda sana kwenda kwenye maonyesho ya Sikinde na Msondo. Nilikuwa nikivutiwa sana na wimbo wa Kassim uliopigwa na Sikinde na sauti ya Gurumo,”alisema mkongwe huyo, aliyeingia nchini mwaka 1978.
Kabeya alisema muziki wa Tanzania unapendwa sana nchini Congo na kuna wakati alipokwenda huko kwa mapumziko, alilazimika kuacha nyumbani kanda za kaseti za Tuncut, Msondo, Sikinde na Maquiz kutokana na rafiki zake wengi kuzigombea.
Mwanamuziki huyo mkongwe aliletwa nchini na wanamuziki Kikumbi Mwanza Mpango ‘King Kikii’ na Nguza Vicking na kujiunga moja kwa moja na bendi ya Maquiz.
Hata hivyo, alishindwa kudumu kwenye bendi hiyo kutokana na kile alichodai kuwa, kutofautiana na viongozi wake kuhusu maslahi. Alisema hali waliyoikuta Maquiz ilikuwa tofauti na alivyoelezwa.
Baada ya kuondoka Maquiz, alijiunga na Orchestra Safari Sound (OSS) wakati huo ikiwa chini ya Kikii na baadaye Fred Ndala Kasheba. Akiwa OSS, alijipatia umaarufu mkubwa kutokana na kibao chake cha Ziada.
Kabeya alisema aliutunga wimbo huo akiwa ndani ya gari, akielekea mazoezini na kwamba lengo lake lilikuwa ni kuacha kumbukumbu ya kudumu. Kabeya aliimba wimbo huo mwanzo hadi mwisho.
Kwa sasa, Kabeya yupo kwenye bendi ya La Capital ‘Wazee Sugu’, inayoundwa na baadhi ya wanamuziki wakongwe wa hapa nchini na kutoka Congo.

No comments:

Post a Comment