'
Thursday, August 11, 2011
Majaliwa aanza kuonyesha cheche Sikinde
MWIMBAJI mpya wa bendi ya muziki wa dansi ya Mlimani Park Orchestra, Shukuru Majaliwa ameibuka na wimbo wake mpya wa kwanza ndani ya bendi hiyo, unaokwenda kwa jina la ‘Fadhila ya punda mateke.’
Majaliwa ametunga wimbo huo, ikiwa ni wiki chache tangu alipojiunga na bendi hiyo, inayotumia miondoko ya Sikinde, akitokea bendi ya Msondo Ngoma.
Akizungumza mjini Dar es Salaam wiki hii, mmoja wa viongozi wa bendi hiyo, ambaye hakupenda jina lake litajwe gazetini alisema, tayari wimbo huo umeshaanza kufanyiwa mazoezi.
Kwa mujibu wa mwanamuziki huyo, kibao hicho kitaanza kusikika rasmi wakati wa sikukuu ya Idi.
“Wimbo huu ni miongoni mwa nyimbo mpya, ambazo tumekuwa tukizifanyia mazoezi katika kipindi hiki cha mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani na tutaanza kuzipiga wakati wa sikukuu ya Idi,”alisema.
Majaliwa amejiunda na Sikinde akiwa ‘deiwaka’ kwa vile ni mwajiriwa wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), akiwa anaitumikia bendi ya Mwenge Jazz ‘Paselepa’.
Mwanamuziki huyo alianza kupata umaarufu baada ya kujiunga na Msondo Ngoma, akiwa ‘deiwaka’, ambapo umahiri wake wa kuiga sauti ya marehemu Moshi William ulimfanye atumike kama mwimbaji ‘kiraka’.
Akizungumza wakati wa utambulisho wake ndani ya Sikinde, Majaliwa alisema ameamua kujiunga na bendi hiyo kwa ridhaa yake mwenyewe na bila ya ushawishi wa mtu yeyote.
Aliongeza kuwa, kabla ya kujiunga na Sikinde, aliwaeleza viongozi wa bendi hiyo sababu za kuondoka kwake Msondo na kuongeza kuwa, walimwelewa ndio maana walimkubalia ombi lake.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment