'
Thursday, August 11, 2011
STELLA: Siwanii taji la Miss Tanzania ili nipate gari
MREMBO wa Kinondoni wa mwaka 2011, Stella Mbuge amesema hawanii taji la mrembo wa Tanzania mwaka huu kwa lengo la kunyakua zawadi ya gari.
Stella amesema anashiriki shindano hilo kwa lengo la kujifunza mambo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kukutana na watu tofauti, kujifunza tabia zao pamoja na mambo yao.
Mwanadada huyo, ambaye pia ni mrembo wa kitongoji cha Tabata, alisema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita alipokuwa akihojiwa katika kipindi cha Jambo Tanzania, kilichorushwa hewani na kituo cha televisheni cha TBC 1.
Stella ni miongoni mwa warembo 30 walioingia kambini mwanzoni mwa wiki hii kwenye jumba la Vodacom House kwa ajili ya maandalizi ya shindano hilo linalotarajiwa kufanyika Septemba 10 mwaka huu mjini Dar es Salaam.
Mrembo huyo alisema, shindano la Miss Tanzania lina maana kubwa kwa warembo zaidi ya kuwania taji na zawadi zingine zinazotolewa kwa washiriki.
“Mimi sishiriki Miss Tanzania kwa kufuata gari. Ninayo mambo mengi ya kujifunza kutokana na shindano hili,”alisema mwanadada huyu.
Stella amesema amepanga kuyatumia mataji yake ya Miss Tabata na Miss Kinondoni kuwahamasisha wasichana katika maeneo ya vijijini kushiriki katika mashindano hayo.
Alisema wapo wasichana wengi wenye sifa za kushiriki mashindano hayo vijijini, lakini hakuna watu wa kuwafuatilia ili kuibua vipaji vyao na kuwaendeleza.
“Mimi binafsi natoka Morogoro Vijijini, wapo wasichana wengi wazuri na wenye sifa za kushiriki mashindano hayo, lakini hawajulikani,”alisema.
“Hivyo moja ya majukumu yangu yatakuwa ni kuwafuatilia wasichana hawa kwa lengo la kuibua vipaji vyao na kuwaendeleza,”alisema.
Mrembo huyo alisema anaona fahari kubwa kuona kila anapopita mitaani, watu wanamnyooshea kidole na kuelezana habari zake. Alisema kwake, hiyo ni faraja kubwa.
Stella alisema hafurahishwi na dhana iliyojengeka miongoni mwa jamii kwamba, mashindano ya urembo ni uhuni. Alisema dhana hiyo imepitwa na wakati kwa vile fani hiyo imewawezesha washiriki wengi kunufaika kimaisha.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment