'
Thursday, August 11, 2011
NCHIMBI: Saidieni michezo mingine
WAZIRI wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Emmanuel Nchimbi ametoa changamoto kwa taasisi, mashirika na watu binasfi kuona umuhimu wa kutoa misaada kwa michezo mingine badala ya soka pekee.
Dk. Nchimbi alitoa changamoto hiyo juzi wakati alipokuwa akikabidhiwa vifaa vya mchezo wa ngumi, vilivyotolewa na Mfuko wa Pensheni ya Watumishi wa Serikali za Mitaa (LAPF) mjini hapa.
LAPF imetoa vifaa hivyo vyenye thamani ya sh. milioni tano kwa Chama cha Ngumi za Ridhaa nchini (BFT) kwa ajili ya timu ya taifa, itakayoshiriki Michezo ya Afrika nchini Msumbiji mwezi ujao.
Waziri Nchimbi alisema vyama vingi vya michezo vinahitaji kupatiwa misaada mbalimbali ili viweze kutekeleza majukumu yake na kuinua viwango vya michezo husika.
“Kwa niaba ya serikali, naishukuru sana LAPF kwa msaada huu wa vifaa vya michezo, ambavyo naamini vitaiwezesha timu yetu ya ngumi kufanya maandalizi mazuri kwa ajili ya michezo ya Afrika,”alisema.
Alitoa mwito kwa mfuko huo, kuandaa bajeti maalumu kuanzia mwakani kwa ajili ya kusaidia maendeleo ya michezo, kama zinavyofanya kampuni na taasisi mbalimbali.
Akizungumza katika hafla hiyo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa LAPF, Don Kida alisema,licha ya mfuko huo kukusanya michango ya wafanyakazi, pia unawajibika kuisaidia jamii ya watanzania. “Kwa maana hiyo, wanamichezo ni sehemu ya jumuia za vijana wetu, ambao kama taasisi, tuna wajibu wa kusaidia kila inapowezekana ili kurudisha sehemu ya mafanikio yanayotokana na utendaji wa mfuko huu”, alisema.
Kida aliyataka mashirika na taasisi zingine, kuiga mfano wao ili ziweze kuchangia maendeleo ya michezo nchini.
Vifaa vilivyotolewa na mfuko huo kwa timu hiyo ni glovu za mikono, vifaa vya kuhami kichwa, padi za mazoezi, viatu vya mazoezi, traki suti, bukuta, fulana za mashindao na vifaa vya mazoezi ya ‘speed ball’.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment