'
Wednesday, June 1, 2016
TFF YASOGEZA MBELE UCHUKUAJI FOMU YANGA
Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), iliyopewa jukumu la kusimamia uchaguzi wa Klabu ya Young Africans imeridhishwa na mwenendo wa wanachama kwa namna wanavyochukua na kurejesha fomu.
Katika kikao chake cha kufanya tathmini kilichoketi jioni ya leo, kamati hiyo chini ya Mwenyekiti wake, Wakili Alloyce Komba, kutokana na mipango yake, imesogeza mbele mchakato wa kuchukua na kurejesha fomu mpaka Jumatatu Juni 6, 2016 saa 10:00 jioni. Isipokuwa Jumamosi na Jumapili ya Juni 4 na 5, 2016.
Hadi sasa wanachama tisa (9) wamechukua na kurejesha fomu. Wanachama hao ni Aaron Nyanda na Titus Osoro wanaowania nafasi ya makamu mwenyekiti kwa mujibu wa katiba ya mwaka 2010 inayotambulika serikalini hadi sasa.
Wengine ni Paschal Laizer, Edgar Chibula, Mohammed Mattaka, Mchafu Ahmed Chakoma, Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’, Omari Said kutoka Zanzibar ambao wanawania nafasi ya Ujumbe wa Kamati ya Utendaji. Uchaguzi wa Yanga unatarajiwa kufanyika Juni 25, 2016.
Fomu zinapatikana katika ofisi za TFF zilizoko Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Ilala jijini Dar es Salaam. Vilevile utaratibu unafanyika ili fomu ziweze kupatikana katika tovuti ya shirikisho www.tff.or.tz
Fomu zinapatikana kwa gharama ya Sh 200,000 kwa nafasi ya mwenyekiti na makamu mwenyekiti na Sh 100,000 kwa wagombea wa nafasi ya ujumbe wa kamati ya utendaji. Mwisho wa kuchukua na kurejesha fomu ni tarehe 6 Juni, 2016.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment