'
Friday, February 28, 2014
WACHEZAJI YANGA KUZOA MIL 100/-, KILA BAO KUNUNULIWA KWA MILIONI MOJA
WAKATI kikosi cha timu ya soka ya Al Ahly ya Misri kimewasili Dar es Salaam kiunyonge, uongozi wa Yanga umewaahidi wachezaji wake kitita cha sh. milioni 200 iwapo watawafunga wapinzani wao.
Mbali na zawadi hiyo ya jumla kwa timu nzima, uongozi wa Yanga umeahidi kutoa sh. milioni moja kwa kila mchezaji atakayefunga bao katika mechi hiyo.
Yanga inatarajiwa kumenyana na Al Ahly keshokutwa katika mechi ya awali ya raundi ya pili ya michuano ya klabu bingwa Afrika, itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Habari zilizopatikana jana kutoka ndani ya uongozi wa Yanga zimeeleza kuwa, ahadi hiyo ya pesa imelenga kuwaongezea ari wachezaji ya kucheza kwa kujituma na hatimaye kushinda mechi hiyo.
Awali, uongozi wa Yanga ulipanga kuwazawadia wachezaji wa timu hiyo sh. milioni 100 iwapo watashinda mechi hiyo, lakini umeamua kuongeza zawadi kwa lengo la kuwaongezea ari zaidi ya kuonyesha maajabu.
Kikosi cha Yanga chenye wachezaji 25, kikiwa chini ya Kocha Hans Van der Pluijm, kimeweka kambi kwenye hoteli ya Bahari Beach iliyoko nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam kwa ajili ya kujiandaa kwa mechi hiyo.
Yanga ilianza mazoezi juzi jioni kwenye uwanja wa Kaunda yaliko makao makuu ya klabu hiyo na jana asubuhi iliendelea kujifua kwenye uwanja wa Boko Beach.
HANS ATAMBA
Akihojiwa na tovuti ya Yanga jana, Hans alisema anashukuru vijana wake wote wapo katika hali nzuri na kwamba hadi sasa hakuna mchezaji majeruhi.
Hans alisema wanatambua mchezo wao dhidi ya Al Ahly, ambao ni mabingwa watetezi wa michuano hiyo, utakuwa mgumu kwa vile wapinzani wao wana uzoefu mkubwa wa michuano ya kimataifa.
"Hakuna kinachoshindikana katika soka, nimewahi kucheza nao nikiwa Ghana katika timu ya Berekum Chelsea katika hatua ya makundi ya robo fainali, hivyo nawajua vizuri jinsi wanavyocheza na kocha Mkwasa alipata fursa nzuri ya kuwaona wiki iliyopita, hivyo naamini mambo yatakuwa mazuri,"alisema kocha huyo kutoka Uholanzi.
Hans alisema lengo la Yanga ni kuweka historia ya kushinda mchezo wa keshokutwa na wa marudiano na kwamba, kikubwa ni kukiandaa kikosi chake kiakili, morari, umoja na nidhamu ya ndani na nje ya uwanja.
WAARABU KIMYAA
Wakati huo huo, kikosi cha wachezaji 22, maofisa wanane wa benchi la ufundi na viongozi watano wa Al Ahly, kiliwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere mjini Dar es Salaam jana kwa ajili ya mechi dhidi ya Yanga.
Kikosi hicho kilitua uwanjani hapo alfajiri ya saa 11.45 kwa ndege ya Shirika la Ndege la Misri na kupanda kwenye basi aina ya Yutong lenye namba za usajili T 391 CRT lililokuwa na maandishi ya Kakote Trans na kupelekwa moja kwa moja kwenye hoteli ya Hyatt Kempsinki.
Hakuna kiongozi yeyote wa timu hiyo ya Misri aliyekuwa tayari kuzungumza na waandishi wa habari wachache waliokuwepo uwanjani hapo. Viongozi na wachezaji wa timu hiyo walitoka nje ya uwanja wakiwa kimya.
Al Ahly imepanga kufanya mazoezi yake jana na leo jioni katika uwanja wa IST ulioko Upanga na kesho jioni itafanya mazoezi yake ya mwisho kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika pambano la keshokutwa kati ya Yanga na Al Ahly.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Kimataifa ya Yanga, Seif Ahmed 'Magari', alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, Membe anatarajiwa kutua nchini keshokutwa asubuhi kutoka nje ya nchi.
Magari alisema waamuzi wa mchezo huo kutoka Ethiopia walitarajiwa kutua nchini jana usiku kwa ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia.
Aliongeza kuwa, uongozi wa Yanga kwa kushirikiana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Jeshi la Polisi mkoa wa Dar es Salaam, wameandaa ulinzi mkali ili kudhibiti vitendo vya vurugu wakati wa mchezo huo.
Magari alisema pia kuwa, kambi ya Yanga iliyoko hoteli ya Bahari Beach, imewekwa chini ya ulinzi mkali ili kuhakikisha wachezaji hawapati bughudha kutoka kwa mashabiki na jamaa zao.
Tiketi za mchezo huo zinatarajiwa kuanza kuuzwa leo Jijini Dar es Salaam katika vituo 10 vilivyotengwa maalumu kwa kazi hiyo.
Ofisa Habari wa Yanga, Baraka Kizuguto amesema kiingilio cha juu kwa VIP A kitakuwa sh. 35,000 wakati VIP B na C ni sh. 25,000.
Viti vya rangi ya chungwa ni sh. 13,000 na viti vya bluu na kijani ni sh. 7000. Mashabiki wameombwa kununua tiketi hizo katika sehemu zilizotangazwa.
Vituo vya mauzo ya tiketi hizo ni makao makuu ya klabu hiyo mitaa ya Twiga na Jangwani, Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Kidongo Chekundu, Buguruni, Uwanja wa Taifa, Dar Live, Stears, Ubungo, Kituo cha Mabasi Mbezi Mwisho na Mwenge.
Tiketi hizo zitakuwa na vipande vinne, ambapo kipande kimoja kitabaki kwa muuzaji, cha pili getini, cha tatu upande anaokaa shabiki na cha nne kitabaki kwa shabiki mwenyewe ili kuepuka kuingia watu zaidi ya wawili kwa kutumia tiketi moja.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment