KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, February 28, 2014

TWIGA STARS KULIPA KISASI KWA WAZAMBIA LEO?



TIMU ya soka ya Taifa ya Wanawake, Twiga Stars inashuka dimbani kesho kumenyana na Zambia katika mechi ya marudiano ya raundi ya kwanza ya michuano ya kuwania ubingwa wa Afrika.

Twiga Stars itashuka dimbani kwenye Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam, ikiwa na kumbukumbu ya kuchapwa mabao 2-1 na Zambia katika mechi ya awali iliyochezwa wiki iliyopita mjini Lusaka.

Ili iweze kusonga mbele katika michuano hiyo, Twiga Stars inahitaji ushindi wa aina yoyote, ikiwa ni pamoja na wa bao 1-0, ambao utaiwezesha kutinga raundi ya pili kwa faida ya bao la ugenini.

Iwapo Twiga Stars itafungwa ama kutoka sare ya aina yoyote, itakuwa imeaga michuano hiyo. Twiga Stars imewahi kucheza fainali za michuano hiyo mara mbili na kutolewa hatua ya awali.

Kikosi cha Zambia kikiwa na wachezaji 18 na viongozi saba, kinatarajiwa kuwasili nchini leo mchana kwa ndege ya Shirika la Ndege la Zambia kwa ajili ya mechi hiyo.
Kocha Mkuu wa Twiga Stars, Rogasian Kaijage, alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, kikosi chake kimejiandaa vyema kushinda mechi hiyo kwa lengo la kusonga mbele.
Kaijage alisema hakuna majeruhi kwenye kikosi chake na wachezaji wote wana ari kubwa ya kulipa kisasi cha kufungwa na Zambia ugenini.
Nahodha wa timu hiyo, Fatuma Mwasikili alisema wamejiandaa vyema kushinda mechi hiyo na amewaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi kuwashangilia ili kuwaongezea nguvu.
Kwa mujibu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), hakutakuwa na kiingilio katika mechi hiyo, lengo kubwa likiwa kupata mashabiki wengi wa kuishangilia Twiga Stars kwa lengo la kuipa nguvu.
Mechi hiyo itakayoanza saa 10 jioni, itachezeshwa na waamuzi Ines Niyonsaba, Jacqueline Ndimurukundo, Axelle Shikana na Suavis Iratunga kutoka Burundi. Waamuzi hao walitarajiwa kuwasili nchini jana jioni.
Kamishna wa mechi hiyo atakuwa Fran Hilton Smith kutoka Afrika Kusini, ambaye anatarajiwa kutua nchini leo asubuhi kwa ndege ya Shirika la Ndege la Afrika Kusini.

No comments:

Post a Comment