'
Friday, February 28, 2014
22 WAITWA TAIFA STARS, KIM POULSEN AFUNGASHIWA VIRAGO
NA AMINA ATHUMAN
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limetangaza kikosi chenye wachezaji 22 kitakachoivaa Namibia katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa uliopo kwenye kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA), bila ya kumshirikisha Kocha Mkuu wa timu hiyo, Kim Poulsen.
Stars na Nambia zitashuka dimbani Machi 5 mwaka huu, katika mchezo utakaofanyika jijini Windhoek, Namibia.
Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura, alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, timu hiyo ilichaguliwa na Kamati ya Utendaji ya TFF iliyokutana hivi karibuni.
Wambura alisema mbali ya kamati hiyo kuteua kikosi hicho, itatangaza ndani ya saa 48 jina la kocha atakayeifundisha timu hiyo kuelekea mchezo huo.
Alisema timu hiyo itaingia kambini keshokutwa kwenye hoteli ya Accommondia na kufanya mazoezi ya siku mbili kabla ya kuondoka nchini Machi 3 mwaka huu kwenda Windhoek.
Aliwataja wachezaji wanaounda timu hiyo kuwa ni makipa Deogratius Munishi (Yanga), Ivo Mapunda (Simba) na Mwadini Ally (Azam). Mabeki wa pembeni ni Edward Charles (JKT Ruvu), Erasto Nyoni (Azam), Hassan Mwasapili (Mbeya City) na Michael Aidan (Ruvu Shooting).
Wengine ni mabeki wa kati, Aggrey Morris (Azam) na Kelvin Yondani (Yanga) wakati viungo ni Amri Kiemba (Simba), Athuman Idd (Yanga), David Luhende (Yanga), Frank Domayo (Yanga), Jonas Mkude (Simba) na Mwinyi Kazimoto (Markhiya Sports Club, Qatar).
Pia wamo washambuliaji Athanas Mdamu (Alliance Mwanza), Haruna Chanongo (Simba), Khamis Mcha (Azam), Mbwana Samata (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC), Mrisho Ngasa (Yanga), Ramadhan Singano (Simba) na Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC).
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment